ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, June 5, 2024

MHASIBU JIJI LA MWANZA AFARIKI AJALINI AKIENDA KWENYE MAZISHI

 


Mhasibu wa Idara ya Mapato ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Amon Joseph (41) amefariki dunia katika ajali ya gari akienda kwenye maziko ya baba mzazi wa mhasibu mwenzake, yaliyotarajiwa kufanyika leo wilayani Kwimba mkoani hapa.


 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kifo cha mhasibu huyo akitaja chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva.


“Ni kweli imetokea ajali hiyo Saa 5:45, maeneo ya Kijiji cha Malembe Kata ya Igongwa Tarafa ya Ngudu Wilaya ya Kwimba kwenye barabara ya vumbi ya Mwabuki kuelekea Jojiro, gari aina ya Toyota Progress lililokuwa likitokea Mwabuki kwenda Ngudu ilimeacha njia na kutumbukia darajani na kusababisha kifo cha dereva (Amon),” amesema Kamanda Mutafungwa.


Awali, Ofisa Mawasiliano wa Halmshauri ya Jiji la Mwanza, Martine Sawema amesema Amon amefariki akiwa safarini kwenda kuhudhuria maziko ya baba mzazi wa mhasibu mwenzake Ngudu wilayani Kwimba.


“Nimeumizwa sana na kifo cha Amon, kiukweli baada ya kufika eneo lile nilichokiona nadhani hata kukosekana na alama za barabara zinazotoa tahadhari kwa madereva kuwa kuna daraja eneo lile kumechangia ajali hii kutokea. Niwaombe Tarura waweke alama katika barabara ile.”


“Pale inaonekana kama alishika breki kama hatua 50 hivi, lakini gari likapinduka hadi kwenye daraja ambalo limejaa maji na hakukuwa na winchi ya kulinyanyua, kwa hiyo amekufa akiwa ndani ya gari. Tumeshautoa mwili na kwenda kuuhifadhi Hospitali ya Bugando,” amesema Sawema.


Akimzungumzia Amon, Kocha wa mpira wa kikapu mkoani Mwanza, Rajabu Kabonga amesema alikuwa mchezaji mwenye upendo ambaye alitamani kuona watoto wakichipukia na kufikia mafanikio katika mpira wa kikapu.


“Alikuwa anacheza Basketball hapo Mirongo, pia alikuwa mwalimu na mchezaji mwenzangu, bado alikuwa na miaka kama mitatu ya kucheza basketball, alikuwa anasifika kuwa na upendo. Ndiyo kocha wa timu ya mpira wa Kikapu ya Profile mkoani Mwanza, tutamkumbuka,” amesema Kabonga.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.