Jeshi la Polisi lingependa kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizoandikwa na kusambazwa kupitia vyombo vya habari zikisema "Wachepusha mfumo wa malipo".
Taarifa hiyo imeenda mbali zaidi ikidai na kutaka kuaminisha umma kuwa askari wa Usalama barabarani wameingilia mfumo wa malipo ya fedha za serikali POS (Point of Sale) na kuchepusha fedha zilizotakiwa kuingia kwenye mfuko mkuu wa serikali. Kilichopo na kilichosahihi ni kwamba Jeshi la Polisi mbali na kuwa na mpango kazi na mikakati ya kutekeleza majukumu yake, hufanya usimamizi na ukaguzi wa namna Askari wanavyotekeleza majukumu yao ili kubaini ufanisi au ukiukwaji wowote ule. Katika ukaguzi uliofanyika hivi karibuni ilibainika baadhi ya Askari walitumia mashine za kupima mwendokasi (,speed radar) kinyume na maelekezo ya Jeshi la Polisi. Baada ya kubainika walichukuliwa hatua za kinidhamu kwa kushtakiwa ambapo nane walishafukuzwa kazi na kufutwa Jeshini na wengine kesi zao zipo katika hatua za mwisho. Hivyo mashine zilizotumiwa kinyume cha utaratibu kwa utashi na kwa manufaa binafsi ya hao askari ni za kupima mwendokasi na si zile zinazotumika kwa ajili ya malipo ya serikali (POS) kwani kuingilia mfumo huo si rahisi kama inavyoelezwa. Mashine aina ya (POS) zinazotumika kwa malipo ya faini za barabarani hadi sasa uchunguzi haujabaini kwamba mfumo wa mashine hizo umeingiliwa na fedha kuchepushwa kama ilivyodaiwa. Jeshi la Polisi linaendelea kusisitiza kwa baadhi ya Waandishi wa Habari wanapoambiwa wasubiri ufuatiliaji unafanyika na taarifa sahihi itatolewa wawe na uelewa na subira kwani wasipofanya hivyo ipo hatari ya kutoa taarifa zenye kuleta taharuki kwa umma bila sababu yeyote ile. Imetolewa na: David A. Misime - DCP Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Dodoma, TanzaniaTupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.