ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, January 31, 2024

MADIWANI HALMASHAURI YA MJI KIBAHA WAIOMBA SERIKALI KUWAPATIA MAMLAKA YAO YA MAJI


NA VICTOR MASANGU KIBAHA


Baraza la madiwani katika Halmashauri ya mji Kibaha limeiomba serikali kuwaundia mamlaka yao ya maji safi ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwahudumia wananchi kwa urahisi zaidi na kuondokana na changamoto zinazowakabili.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Kibaha  Mhe Mussa Ndomba kwa niaba ya madiwani wenzake wakati wa kikao cha baraza la madiwani kipindi cha robo ya pili.
Mhe.Ndomba alisema kwamba kwa sasa katika baadhi ya maeneo kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama hali ambayo inawapa wakati mgumu wananchi kupata huduma hiyo.

Alifafanua kwamba katika halmashauri ya mji kibaha kuna Hospitali ya Lulanzi ambayo ni ya Wilaya lakini nayo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji hususa kwa wakinamama wanaojifungua kupata shida sana.
"Kutokana na hali hii ya changamoto ya maji tunaiomba serikali kutusaidia katika halmashauri ya Kibaha tuwe na mamlaka yetu ya maji ambayo itakuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wetu ukizingatia maji yote yanatokea kwetu Kibaha,"alifafanua Ndomba.

Aidha Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa endapo Kibaha ikiba ikiwa na mamlaka yake itaweza kusaidia kuwapunguzia wananchi  adha ambayo yamekuwa wakiipata.
Pia alisema kwamba kwa sasa halmashauri ya mji Kibaha imetenga kiasi cha shilingi milioni 60 kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombinu ya maji ili iweze kufika katika Hospitali ya Lulanzi ili wagonjwa waondokane na kuangaika katika suala la maji.

Kadhalika Mwenyekiti huyo aliziomba taasisi wezeshi zote kuwa na ushirikiano wa pamoja katika masuala ya kutekeleza miradi mbali mbali  ya kimaendeleo ili kuepusha usumbufu unaokuwa ukijitokeza katika utekelezaji wa miradi.

 Mwenyekiti huyo alimpongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kulifuta shirika la Elimu kibaha na kumuomba awapatie ardhi kutoka eneo hilo kwa ajili ya kulipanga na matumizi mengine ya kimaendeleo.

"Kiukweli Rais wetu amesikia kilio chetu cha siku nyingi kwa kuamua kulifuta shirika la elimu Kibaha na sisi siku nyingi kama madiwani tulikuwa tunaomba kupatiwa eneo kwa lengo la shughuli mbali mbali lakini hatukuweza kulipata,"alibaisha Ndomba.

Katika hatua nyingine Ndomba aliwataka watumishi na watendaji kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kusimamia kumaliza  migogoro ya ardhi.

"Kero nyingi zinazokuja ni kuhusiana na migogoro ya ardhi ya wakati mwingine unakuta mkurugenzi anashughulikia migogoro hiyo ya ardhi ya asilimia 90 kitu ambacho kilitakiwa kimalizike katika ngazi za chini sio hadi ifike kwa mkuu wa Wilaya au mkuu wa Mkoa,"alisema Ndomba.
 Nao baadhi ya madiwani aliohudhuria katika kikao hicho walisema katika maeneo yao kumekuwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara hasa katika kipindi cha mvua hivyo mamlaka husika zinapaswa kufanya matengenezo.

Aidha waliongeza kuwa suala la changamoto ya maji bado ni tatizo katika maeneo yao hivyo kuanzishwa kwa mamlaka yao kutaweza kuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi.

Kikao cha baraza la madiwani katika halmashauri ya mji Kibaha kimekutana katika robo ya pili kwa ajili ya kujadili mipango mbali mbali ya kimaendeleo katika sekta tofauti,changamoto zilizopo pamoja na kuweka mikakati ya kuzitafutia ufumbuzi kupitia serikali pamoja na taasisi wezeshi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.