Na Oscar Assenga, TANGA
JESHI la Polisi Mkoani Tanga limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 107 kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya Mauaji,Wizi ya Mifugo,Unyang’anyi wa kutumia silaha ,kuingia nchini bila kibali pamoja na kupatikana dawa za kulevya aina mbalimbali.
Hayo yalisemwa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Jijini Tanga kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Octoba hadi Novemba 27, 2023.
Kamanda Mchunguzi alisema kwamba kati ya watuhumiwa hao 21 wamekamatwa na Bhangi kilogramu 43, Mirungi Kilogramu 124,
Heroin Gramu 242 huku wanne (4) wakikamatwa kwa kosa la kusafirisha wahamiaji haramu na watuhumiwa saba (7) raia wa Ethiopia kuingia nchini bila kibali.
Aliwataja wengine ni mtuhumiwa 01 kupatikana na kosa la unyang’anyi kwa kutumia silaha aina ya Panga na watuhumiwa wengine 74 wamekamatwa huku upelekezo ukiwa bado unaendelea.
Aidha Kamanda Mchunguzi alisema pia katika kuimarisha doria za nchi kavu na baharini Novemba 21 mwaka huu huko maeneo ya Kisiwa cha Jambe wilaya ya Tanga walifanikiwa kukamata boti aina ya Fibre yenye rangi nyeupe na bluu isiyokuwa na usajili ikiwa na injini ya Yamaha HP 15.
Alisema vitu nyengine vilivyokuwepo kwenye boti hiyo ni Chupa za Hewa ya Oxygen 02,(Diving Cylinder),mipira ya kupumulia 02 (regulator),Tega ya kuokotea Samaki,Kiberiti 01 na Samaki aina mbalimbali Kilogramu 30 waliovuliwa kwa kutumia baruti ambao walithibitishwa na Afisa Uvuvi kuwa hawafai kwa matumizi ya Binadamu.
Aliongeza kwamba watuhumiwa wamekimbia na kutelekeza boti hiyo baada ya kugundua wanafuatiliwa na Polisi wa Kikosi cha Wanamaji Tanga huku Upelelezi unaendelea kwa kuwatafuta watuhumiwa wa tukio hilo.
Hata hivyo Kamanda Mchunguzi alitaja tukio lingine kuwa ni Novemba 18 mwaka huu Jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata Hamisi Kombo (46) mkazi wa Kwediboma wilaya ya Kilindi akiwa na wenzake nane .
Alisema wenzake wote hao ni waganga wa kienyeji ambao wanajihusisha na rasmi chonganishi wakiwa katika kijiji cha Kivindani Kata ya Tongoni Tarafa ya Pongwe wilaya ya Tanga ambapo wananchi wa eneo hilo waliwaita waganga hao kwa ajili ya kufanya ukaguzi katika nyumba za kijiji hicho ambazo zinasadikiwa kuwa na uchawi.
Kamanda huyo alisema uchawi huo ambao wanajiji hao walilalamika kuwa wakitendewa vitendo vya kudhalilishwa kwa kuvuliwa nguo na kuachwa wakiwa watupu kimazingara wakati wakiwa wamelala usiku,ambao watuhumiwa hao wote wapo nje kwa dhamana wakati upelelezi wa shauri hilo ukiendelea.
Katika hatua nyengine Kamanda Mchunguzi alisema katika kipindi mwezi mmoja Jumla ya watuhumiwa 41 wamefikishwa mahakamani,kesi 11 zinaendelea mahakamani na kesi 27 zimetolewa hukumu mbalimbali ambapo watuhumiwa watatu ambao ni Justis Kunael(40),Saidi Adam (32) na Maliki Amiri (38) wote wakazi wa Handeni wamehukumiwa kifungo cha Maisha kwa kosa la kubaka.
Kwenye tukio la Mauaji,Kamanda Mchunguzi alisema watuhumiwa Rashid Mwalimu “Chidi Kiwangwa”(32),Siwajui Kigaa “Sahonelo” (27) na Zuberi Hassani (34) wote wakazi wa Kijiji cha Kwandugwa wilayani Handeni walihukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji ya mtoto wa Kike mwenye umri wa miaka (9).
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.