ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, May 3, 2023

UWT KIBAHA YAJA NA MPANGO WA KUPAMBANA NA VITENDO VYA UKATILI KWA WATOTO WA KIKE.

 


Na  Victor Masangu,Kibaha 


Mwenyekiti wa umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mji Elina Mgonja amekemea vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wa kike hususan  baadhi ya wanafunzi kubakwa.

Mgonja ameyasema hayo kwa wakati ziara yake ya kikazi katika kata mbili za Tangini pamoja na kata ya Tumbi ikiwa ni kwa ajili ya kutembelea wanachama pamoja na kuangalia mwenendo mzima wa uhai wa chama na kuzungumza na wanawake wa ngazi mbali mbali.


Mwenyekiti huyo ambaye katika ziara hiyo ameambatana na viongozi mbali mbali wa chama pamoja na viongozi wa jumuiya mbali mbali kuanzia ngazi za matawi hadi ngazi ya Wilaya sambamba na wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya UWT pamoja na mlezi wa jumuiya hiyo  mama Selina Koka.

Mgonja amesema anachukizwa kuona baadhi ya wanafunzi kufanyiwa vitendo vya ubakaji hasa katika kipindi cha asubuhi wanapokwenda shule wanakutana na vijana ambao sio watu wazuri na kuamua kuwabaka.

"Kwa kweli vitendo vya ukatili pamoja na ubakaji kwa kweli vimezidi na hii ni kutokana na taratibu ambazo zimewekwa na baadhi ya shule za kutaka wafike shule muda wa saa kumi na mbili asubuhi kwa hivyo inawalazimu waamke asubuhi sana kwa kweli hii sio sahihi ,"alisema Mgonja.

Aidha aliwataka madiwani Kuhakikisha wanaliingilia kati sakata hili na kulifikisha katika mamlaka zinazohusika ili liziwe kufanyiwa ufumbuzi na kwamba na yeye atolifumbia macho atalifanyia kazi endapo viongozi husika watashindwa kulitafutia ufumbuzi wa haraka.

"Jambo hili linaumiza kweli sisi hatuwezi kulifumbia macho kabisa hata kidogo ni lazima sisi kama  wazazi na walezi tushikamane kwa pamoja ili wahusika wa hizo shule waweze kupanga muda mzuri wa kuwasili shuleni hata saa moja na nusu kunakuwa tayari kumeshakucha na Kuna mwanga,"aliongeza Mgonja.

Katika hatua nyingine aliwahimiza wazazi na walezi kujenga utaratibu wa kuwakagua watoto wao mara kwa mara ili kuweza kuwabaini kama wanafanyiwa vitendo vya ubakaji na kuwataka kuwafichua wale wote ambao wanahusika na vitendo hivyo.


Mlezi wa jumuiya hiyo ya UWT Selina Koka ambaye ni mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini amesema ataendelea kuwashika mkono katika kuwasaidia wanawake pamoja na kupinga vikali vitendo vya ukatili kwa wanawake na wasichana.

Nao baadhi ya madiwani wa viti maalumu katika halmashauri ya mji Kibaha ambao wameambatana katika ziara hiyo wamesema watalivalia njuga suala hilo la unyanyasaji wa kijinsia pamoja na baadhi ya wanafunzi kubakwa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.