ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, May 5, 2023

BENKI YA CRDB YAWAHAKIKISHIA WANAWAKE WAJASIRIAMALI MTAJI WA BIASHARA

 


Siku mbili baada ya Benki ya CRDB kupata leseni ya kutoa huduma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amewahikikishia wanawake wajasiriamali nchini kupata mtaji wa kuanzisha au kukuza miradi yao.
 
Mwambapa ametoa uhakika huo leo jijini Dar es Salaam alipozungumza na wanawake wanachama wa Buta Vicoba kwenye mafunzo waliyokuwa wanapewa katika ukumbi wa Ngome uliopo Mwenge.

“Tukiwa Benki kiongozi na ya kizalendo, tumekuwa mstari wa mbele kuyawezesha kiuchumi makundi mbalimbali katika jamii yetu mkiwamo wanawake kupitia huduma, bidhaa na program bunifu. Benki inatoa mikopo maalum ya wanawake na mafunzo na hadi mwishoni mwa mwaka 2022 Benki ilikuwa imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 112 na kuwapa mafunzo wanawake wajasiriamali zaidi ya 14,774,” amesema Bi Mwambapa.
Pamoja na uwezeshaji wa huduma za fedha kwa wanawake, Mwambapa amesema Benki iliona bado kuna kundi kubwa la wanawake ambalo huduma zilizopo haziwezi kuwawezesha kujikwamua kiuchumi hasa wale ambao wana biashara au mawazo ya biashara lakini hawawezi kuingia katika mfumo rasmi wa huduma za fedha kutokana na kutokidhi baadhi ya vigezo hivyo wakaona wawahudumie kupitia sera yao ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI Policy) katika maeneo ya kipaumbele katika uwekezaji kwa jamii inaayotekelezwa na CRDB Bank Foundation kupitia program ya Imbeju.

Programu ya Imbeju inalenga kuwawezesha wanawake kukuza biashara zao ili kujikwamua kiuchumi wao na familia zao ili watoe mchango kwa Taifa kupitia kodi za biashara na kuwaajiri Watanzania wengine watakaojikwamua kupitia ajira hizo.

“Ili kuhakikisha programu hizi zinakuwa endelevu na zenye matokeo makubwa, CRDB Bank Foundation inajenga jukwaa shirikishi linalowaleta pamoja wadau wa maendeleo ndani na nje ya nchi. Ukiwa hapa una uhakika wa kupata elimu ya fedha Pamoja na mtaji wa kufanyia biashara yako,” amesema Bi Mwambapa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Buta Vicoba, Semeni Gama ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuwapa mafuno zaidi ya wanachama wake 300 kutoka vikundi vinavyounda umoja wao waliojitokeza huku akiwasihi waache kubweteka badala yake wajielekeze katika kujijenga kiuchumi.

Mwanzoni mwa wiki hii Benki ya CRDB imepewa leseni ya kufanya biashara nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) baada ya kukamilisha hatua zote zinazohitajika hivyo kuwa benki ya kwanza ya kizalendo kuwahudumia Wacongo.

Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, Benki ya CRDB iliyoanzishwa mwaka 1996 inatoa huduma zake nchini Burundi pia.
 



Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.