MAPEMA asubuhi ya leo Jumapili ya tarehe 6 November 2022 mara baada ya ajali wananchi wameonekana eneo la tukio wakitumia nguvu zao kuivuta kwa kamba ndege ya Shirika la Precision Air toka kwenye maji Ziwa Victoria kuelekea ufukweni.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amesema watu 26 kati ya 43 waliokuwa kwenye ndege ya Shirika la Precision Air iliyopata ajali Ziwa Victoria, mjini Bukoba mkoani Kagera, wameokolewa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 6, 2022 mjini Bukoba, Chalamila amesema ndege hiyo ilikuwa na jumla ya watu 43 ambapo kati yao 39 ni abiria, wahudumu wawili na marubani wawili.
Amesema ndege hiyo iliyopata ajali leo ikiwa inatoka jijini Dar es Salaam kwenda mjini Bukoba.
“Leo tumepata majanga ya ndege ya Precision Air ambayo ilikuwa inatoka Dar es Salaam kuja Bukoba.
Ilikuwa na jumla ya watu 43 ambapo kati ya hao, 39 ni abiria, wawili ni wahudumu na wawili marubani,” amesema Chalamila.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo muda mfupi baada ya ajali hiyo, inasema ndege hiyo aina ya PW 494 iliyokuwa imeruka kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba ilipata ajali muda mfupi kabla ya kutua uwanja wa ndege wa Bukoba.
“Ndege ya Precision Air namba PW 494 iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Bukoba ilipata ajali muda mfupi kabla ya kutua Uwanja wa Ndege wa Bukoba,” inaeleza taarifa ya shirika hilo huku likiahidi kutoa taarifa kamili baadaye.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.