ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, November 24, 2022

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Burundi aipongeza Benki ya CRDB Burundi kwa miaka 10 ya Mafanikio

 

Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni Mama ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (watatu kulia) akikabidhi tuzo maalumu ya shukrani ya maadhimisho ya miaka 10 ya kampuni tanzu ya Benki ya CRDB Burundi kwa Naibu Gavana wa kwanza Benki Kuu ya Burundi, Desire Musharitse (katikati) pamoja na Naibu Gavana wa pili, Marie Goreth Ndayishimiye. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Burundi, Hosea Kashimba (wapili kulia), Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wapili kushoto), Mkurugenzi wa Benki ya CRDB Burundi, Fredrick Siwale (kushoto) pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Burundi, Menard Bucumi.

=========   ========   ========

Bujumbura, 24 Novemba 2022 – Benki Kuu ya nchini Burundi (BRB) imeipongeza Benki ya CRDB Burundi kwa mafanikio makubwa iliyopata katika kipindi cha miaka 10 ya uwepo wake nchini Burundi. 

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Gavana wa Kwanza wa Benki Kuu ya Burundi kwa niaba ya Gavana katika mkutano na ujumbe wa Benki ya CRDB ulioongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela aliyeambatana na wajumbe wa Bodi ya kampuni Mama ya Benki ya CRDB pamoja na kampuni tanzu ya Benki ya CRDB Burundi. Ujumbe huo umetembelea Benki Kuu ya Burundi kutoa shukrani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya utoaji huduma za kibenki ya kampuni tanzu ya Benki ya CRDB Burundi.
Akizungumza katika mkutano, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Burundi, Desire Musharitse alisema Benki Kuu ya nchi hiyo inafurahia sana kwa uwepo wa Benki ya CRDB nchini Burundi kwani imekua sehemu ya uwezeshaji wa miradi mingi ya kiuchumi kwa nchi lakini pia imechangia uwezeshaji wa wafanyabiashara.

“Tulipata matatizo yaliyopelekea changamoto kubwa ya upatikanaji wa fedha za kigeni mwaka 2015 lakini tulipata msaada mkubwa sana kutoka Benki ya CRDB na hakika hilo limedhihirisha ule usemi wa rafiki wa kweli hujulikana wakati wa shida” alisema Musharitse.
Tangu ilipoingia katika soko la Burundi mwaka 2012, Benki ya CRDB imekua ikifanya vyema sokoni na katika kipindi cha miaka 10 tu imeweza kushika nafasi ya tatu kati ya benki kumi na tatu zinazotoa huduma za kibenki nchini Burundi. Katika kipindi hiko Benki imeweza kufungua matawi manne huku tawi la tano likitarajiwa kufunguliwa mapema mwaka 2023.

“Kutokana na kufanya vizuri kwa Benki ya CRDB Burundi tunatamani kuona ikifungua matawi mengi zaidi nje ya Bujumbura lakini pia kuweza kufanikisha upatikanaji wa mikopo kwa njia za kidigitali kama ambavyo wamekua wakitoa huduma nyingine kidigitali” aliongeza Musharitse.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameishukuru Benki Kuu ya Burundi kwa ushirikiano mkubwa kwa Benki ya CRDB Burundi uliopelekea kampuni tanzu hiyo kupata mafanikio makubwa ndani ya kipindi kifupi cha miaka 10. Sambamba na hilo Nsekela ameishukuru Serikali ya nchi hiyo chini ya Rais Evariste Ndayishimiye kwa kuipatia eneo Benki ya CRDB Burundi katika makao makuu mapya ya nchi ya Gitega ili kufanikisha ujenzi wa tawi jipya.

“Maraisi wetu wanatamani kuona ushirikiano wa sekta binafsi za Tanzania na Burundi lakini pia wamezungumza juu ya miradi ya kimkakati kati ya nchi hizi mbili ikiwemo mradi wa SGR na sisi tuko tayari kuisadia kampuni yetu tanzu kushiriki katika mradi huu kwa upande wa Burundi kama ambavyo tumeshiriki kwa upande wa Tanzania” alisema Nsekela.
Aidha, alisema Benki ya CRDB inatarajia kuingia nchini DRC hivi karibuni jambo ambalo litachangia kukuza biashara kati ya Burundi na DRC lakini pia ushirikiano wa biashara kati ya nchi hizo na Tanzania ambazo kwa pamoja ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Adhma yetu katika masoko tunayohudumia sio tu kutoa huduma bora bali kutoa mchango katika uchumi na kubadilisha maisha ya watu tunaowahudumia hivyo tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na Benki Kuu ya Burundi ili kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini Burundi” aliongeza Nsekela.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Burundi, Hosea Kashimba na yeye alitoa shukrani za bodi kwa Benki Kuu ya Burundi kwa ushirikiano mkubwa uliochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Benki ya CRDB Burundi katika kipindi cha miaka 10 tangu kuingia katika soko la Burundi. 

“Tunaona muelekeo mzuri wa nchi na tunaamini ndani ya kipindi kifupi kijacho tutaweza kuwa Benki kiongozi hapa nchini Burundi hivyo basi tunaomba ushirikiano huu uendelee kwani hatuwezi kufikia malengo yetu bila ushirikiano wenu” alisema Kashimba ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma PSSSF.
Maadhimisho ya miaka 10 ya Benki ya CRDB Burundi yameambatana na shughuli mbalimbali zenye lengo la kushukuru jamii ya watu wa Burundi kuiwezesha Benki ya CRDB Burundi kufanya vizuri sokoni.  Sehemu ya shughuli zilizofanyika ni pamoja na kutoa misaada kwa makundi yenye uhitaji maalum, uandaaji wa shindano la mchezo wa mpira wa kikapu kwa vijana pamoja na ujenzi wa mradi wa usafi kwa jiji la Bujumbura.

Benki ya CRDB Burundi ilianzishwa nchini Burundi mnamo mwaka 2012 chini ya sheria ya makampuni nchini Burundi.  Benki ya CRB Burundi inatoa huduma kwa wateja wa taasisi na makampuni pamoja na wateja binafsi huku ikimilikiwa na kampuni Mama ya Benki ya CRDB kwa asilimia 100. Benki ya CRDB Burundi inatoa huduma kupitia matawi manne sambamba na mawakala wa benki zaidi ya 600. Hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka 2022, Benki ya CRDB Burundi imetoa mikopo ya zaidi ya Faranga Bilioni 300 za Burundi kwa sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, viwanda na utalii.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.