WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua jengo la Idara ya Macho katika Hospitali ya Kanda Bugando ambalo limekuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa kwa kuwarahisishia upatikanaji wa huduma za kibingwa za macho.
“Ujenzi wa mradi huu unakwenda kupunguza usumbufu kwa wagonjwa waliokuwa wakisafiri umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 1,000 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda hospitali ya KCMC au Muhimbili kwa ajili ya kupata huduma bora za macho.”
Waziri Mkuu amezindua jengo hilo jana Jumapili, Oktoba 16, 2022 katika Hospitali ya Kanda Bugando jijini Mwanza akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu kukagua shughuli za maendeleo zinazotekeleza na Serikali mkoani hapa. Mradi huo umegharimu shilingi bilioni 3.7.
Akizungumza na wananchi baada ya kuzindua mradi huo unaolenga Kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma bora za kibingwa na zinazokidhi matakwa na matarajio ya wagonjwa, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini likiwemo Kanisa Katoliki katika kuboresha huduma za jamii yakiwemo matibabu.Mheshimiwa Majaliwa amesema katika Hospitali ya Bugando Serikali imekuwa na ubia na kanisa kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kugharamia mishahara kwa watumishi 1,191 sawa na asilimia 66 ya watumishi wote wa hospitali ambapo kila mwezi jumla ya shilingi bilioni 1.7 hulipwa na Serikali.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.