Polisi katika kaunti ya Muranga wamemkamata mshukiwa anayedaiwa kuwa kiongozi wa genge hatari linalowahangaisha wakazi.
John Ngugi Maina aliviziwa kutoka kwa maficho yake ana afisa aliyejifanya kahaba.
Afisa wa polisi wa kike kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai(DCI) ambaye alijifanya kahaba, alimvizia John Ngugi Maina kutoka kwa maficho yake baada ya kukubaliana kufanya biashara usiku huo.
Ngugi anatuhumiwa kuongoza genge la Jeshi ya Gaica ambalo huendesha oparesheni yake mjini Maragua viunga vyake. Mshukiwa huyo aliwahi kukamatwa mnamo Aprili 21, na kuachiliwa kwa bondi ya KSh 30,000 na Mahakama ya Kigumo.
Alikuwa amekamatwa kwa kutengeneza na kuuza pombe haramu.
Ripoti za polisi zilionyesha kuwa genge hilo la uhalifu hutengeneza na kuuza chang'a na dawa zingine za kulevya.
Nation Africa inaripoti kwamba watu watatu wa genge hilo walikamatwa mnamo Agosti 18 mjini Thika walipofumaniwa baada ya kuwaibia madereva na wasafiri wa miguu wakiwa wamejihami na bastola.
Hati ya kukamatwa ilitolewa dhidi ya Ngugi kwa kukosa kufika kortini kesi yake ilipokuwa ikitajwa mnamo Julai 26, baada ya kupewa dhamana. "Kwa muda wa mwezi mmoja, mwanamume huyu amekuwa akitoroka, maafisa wetu wakapata taarifa za kijasusi kwamba alikuwa akionekana katika nyumba za madanguro mjini lakini kila tulipokuwa tukijitokeza, hakuwepo," Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini Alexander Shikondi alidai.
Mahakama ya Kigumo iliipa kituo cha polisi cha Maragua makataa ya kumkamata mshukiwa huyo kabla ya Septemba 5.
Shikondi alisema ilikuwa vigumu kumkamata kiongozi huyo wa genge la uhalifu kwa sababu alikuwa akihamahama sana. Kamanda huyo wa polisi alifichua kuwa Ngugi angeingia kwenye nyumba za madanguro akitumia pikipiki, na kumpeleka kahaba mmoja kwenye maficho yake na kumrudisha. "Tuliamua kutumia udhaifu wake wa kuwatumia makahaba ili kumnasa," polisi huyo alisema.
Shikondi alisema walimwekea mtego kumnasa baada ya kupata nambari yake ya simu. Afisa wa kike anayehudumu katika makao makuu ya DCI huko Kiambu alitumia nambari hiyo kumpigia mshukiwa na kujitambulisha kama mwanamke ambaye alikutana naye mjini Kenol.
"Tulikuwa tukifuatilia mazungumzo na ingawa alisita kwanza udhaifu wa mwanamke ulimfanya aache kujificha na kukubali kufika mjini kwa mkutano, akionya kwamba hatakaa muda mrefu," Shikondi alisimulia. Mhalifu huyo alijitokeza, akaegesha pikipiki yake na kujitolea kumnunulia vinywaji afisa huyo mpelelezi.
"Alisahau kwamba alikuwa mtoro ... alimwongoza mwanamke 'wake' kwenye baa iliyokuwa karibu na kuitisha vinywaji ... Walikuwa wakijiburudisha na kinywaji chao cha pili kila mmoja wakati maafisa watatu walijitokeza na kumfunga pingu. Sasa yuko rumande na ataanza tena kujitetea katika marejeleo yake ya kesi ya jinai 388/22 katika mahakama ya Kigumo,” akasema.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.