Zahanati ya Mtaa wa Lumala Magharibi iliyozinduliwa leo Aprili 8,2022 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel
*************************
Katika kuhakikisha huduma za afya zinasogea karibu na wananchi milioni 300 zimetumika kukamilisha ujenzi wa Zahanati tatu katika wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.
Fedha hizo zilitolewa na Serikali lengo ikiwa ni kusaidia ukamilishaji wa Zahanati tatu zilizoibuliwa kwa nguvu za wananchini ambazo ni Zahanati mpya ya Mtaa wa Lumala Magharibi, Zahanati mpya ya Mtaa wa Masemele na Zahanati mpya ya Mtaa wa Nyamadoke.
Hafla ya uzinduzi wa Zahanati hizo umefanyika leo Aprili 8,2022 katika Mtaa wa Lumala Magharibi ilipojengwa Zahanati mpya.
Akizungumza mara baada ya kukagua na kuzindua Zahanati ya Lumala Magharibi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, amesema kuwa Zahanati hizo zitasaidia Wananchi kupata huduma ya afya kwa karibu hali itakayo saidia kupunguza vifo vya kina mama na watoto
Amesema Serikali imewekeza mabilioni ya fedha kwa ajili ya kujenga Zahanati,vituo vya afya lengo ni kuokoa maisha ya mama,mtoto na watanzania kwa ujumla.
Gabriel amewaomba wanaume kuwa mabolozi wazuri wa kuwapeleka wake zao kwenda Zahanati kwaajili ya kupata vipimo mbalimbali pindi wanapopata ujauzito.
Aidha amewaomba wakinamama kuachana na tabia ya kutumia mitishamba kipindi cha ujauzito kwa lengo la kuongeza uchungu, badala yake wachukue hatua nzuri na salama za maisha yao kwa kufika kwenye Zahanati kwaajili ya kupata ushauri wa wataalamu wa afya.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa Zahanati hizo kwaniaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela,Mchumi wa Manispaa hiyo Mophen Mwakajonga amesema kuwa Zahanati ya Lumala ilipokea jumla ya fedha milioni 152.2 ambapo kati ya fedha hizo milioni 100 zilitoka Serikali Kuu,milioni 5 zilitoka Halimashauri na milioni 47.2 ni michango ya wananchi,hadi kukamilika kwa mradi huo zaidi ya milioni 151.4 zimetumika, ambapo hadi sasa Zahanati ipo tayari kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wa Zahanati mpya ya Nyamadoke Mwakajonga amesema kuwa mradi ulipokea milioni 133.4 ambapo kati ya fedha hizo milioni 100 zilitoka Serikali kuu, milioni 10 zilitoka Halimashauri na zaidi ya milioni 23.4 ni michango ya wananchi, mradi huo umegharimu zaidi ya milioni 127.8 na hadi sasa Zahanati imeanza kutoa huduma kwa wananchi kwani tangu Aprili 1,2022 hadi Aprili 6,2022 wagonjwa 21 wamehudimiwa.
Akizungumza Zahanati mpya ya Mtaa wa Masemele Mwakajonga amesema kuwa mradi huo ulipokea zaidi ya milioni 113.5 kati ya fedha hizo milioni 100 zilitoka Serikali kuu, zaidi ya milioni 2 zilitolewa na Halmashauri, milioni 10.4 michango ya wananchi,milioni 1.06 zilitolewa na Mh.Mbunge,ujenzi huo umegharimu zaidi ya milioni 113.5 na salio
Mwakajonga amesema kuwa Zahanati za Masemele na Nyamadoke zinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa umeme,upungufu wa vifaa tiba.
Kwaupande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala, amesema kuwa wamekuwa wakikabidhi miradi mingi ikiwemo ya afya kutokana na fedha wanazozipokea kutoka Serikalini.
Amesema watazidi kusimamia kwa uaminifu na umakini mkubwa miradi yote inayotekelezwa katika wilaya yake.
Mary Fungameza ni mkazi wa Mtaa wa Lumala amesema uwepo wa Zahanati hiyo ni faraja kubwa sana kwake kwani anauhakika wa kupata huduma ya afya kwa karibu na kwawakati.
Amesema kipindi cha nyuma walipata shida sana hasa kwa wakina mama walipokuwa wakitaka kujifunga kutokana na kutokuwepo kwa Zahanati katika Mtaa wao hali iliyopelekea mama na mtoto kupoteza maisha kwa kuchelewa kupata huduma.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.