ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, April 20, 2022

WAFANYABIASHARA IRINGA WALALAMIKIA KUTOZWA KODI KUBWA

 

Moja ya barua ambazo wafanyabiashara waliopanga katika jengo la Halmashauri ya Iringa wakituma malalamiko kwa mkuu wa wilaya juu ya kutosikilizwa na ofisi ya mkurugenzi.
Hii ni barua kutoka kwa mkurugenzi akiwaalika wafanyabiashara kwenye kikao cha maridhiano juu ya bei zao



Na Fredy Mgunda,Iringa.

WAFANYABIASHARA waliopanga katika jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa lililopo karibu na Stendi ya zamani ya Mabasi ya Mkoani wamelalamikia kutozwa kodi kubwa kutoka ofisi ya Halmashauri hiyo.

Wakizungumza na waandishi wa habari wafanyabiashara hao walisema kuwa wanalipishwa kodi kubwa kuliko biashara ilivyo katika eneo ambalo kwasasa halina wateja kama ilivyokuwa awali.

Walisema kuwa wamekuwa na majadiliano ya mara kwa mara na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo lakini wamekuwa hawapati ushirikiano wa kutosha kutatua changamoto hiyo.

Raphati kaberege ni mfanyabiashira aliyepanga katika jengo hilo alisema kuwa wameandika barua ya kuomba kukutana na viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Iringa toka mwaka 2017 na hawajawahi kujibiwa.

“Kwa kweli mamlaka hawajahi kutupa ushirikiano licha ya kuwaandikia barua, Pia tumewahi kuwaalika katika eneo la biashara lakini hawajahi kufika, na ukiangalia mazingira ya biashara hayaridhishi kwani vyoo wakati mwingine vimejaa na mitaro imeziba jambo linalohatarisha afya zetu”alisema kaberege

Alisema kuwa wameitwa na mkurugenzi ili kufanya kikao cha majadiliano lakini mkurugezi hakufanikiwa kufika katika kikao hicho ambacho ofisi yake ilikiitisha kwa ajili ya majadiliano.

Kaberege alisema kuwa vyumba vya biashara ambavyo vinapangishwa na halmashauri ya Manispaa ya Iringa na vyumba vya biashara vya CCM Iringa ni gharama nafuu Zaidi kuliko halmashauri ya wilaya ya Iringa.

“Mfano CCM wanalipa wanatoza kiasi cha shilingi 50,000 hadi 70,000 na maeneo mengine yanayotazamana na jengo hilo wafanyabiashara wanalipa kwa gharama ya shilingi laki moja (100,000) hadi laki moja na nusu (150,000) kwa mwezi,tofauti na sisi” alisema kaberege

Isaack Steven ni Miongoni mwa wapangaji katika jengo hilo amesema kuwa kwa wafanyabiashara waliopanga milango ya mbele wanalipa shilingi laki tatu na nusu (350,000) huku waliopanga milango ya nyuma wakitozwa kodi ya shilingi laki Moja (100,000).

Alisema kuwa kodi hizo ni kubwa sana kwa kuwa eneo hilo kwa sasa halina mzunguko wa biashara baada ya standi kuhamishiwa eneo la igumbilo ambapo pia mazingira ya jengo hilo siyo rafiki kwani choo wanachotumia wanatozwa fedha nyingi.

Mfanyabiashara Alice Ngwale alisema kuwa licha ya kuchajiwa fedha kubwa ya pango ya mwezi pia wanashindwa kuendesha biashara zao kwani wamekuwa wakitoa fedha katika vyanzo vingine vya mapato ili waweze kulipia majengo hayo.

Wapangaji hao kwa kauli moja waliamua kuondoka katika Ofisi za Siasa ni kilimo baada ya Mkurugenzi wa halmashauri kushindwa kufika katika kikao hicho huku wakiiomba serikali kuwawekea utaratibu mzuri wa kulipa kodi kila mwezi au kila baada ya miezi mitatu na siyo kila baada ya miezi 6 jambo ambalo linawafanya washindwe kumudu gharama hizo.

 

 

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Stephen Mhapa alisema kuwa kama wanaona kuwa kodi waliyopangiwa ni kubwa bora wakaachia vyumba hivyo kwa kuwa wanafanya biashara sio kutoa huduma kwa wananchi.

Mhapa alisema kuwa hata ukienda kwa watu binafsi inaendana na gharama ambazo halmashauri inapangisha kwa wafanyabiashara waliopanga katika jengo hilo.

Alisema kuw malalamiko ya kushuka kwa biashara hayana mashiko kwa kuwa changamoto hiyo ipo na bado wafanyabiashara wengine wa jirani wanafanya biashara kwanini wawe wao.

Mhapa alimazia kwa kusema kuwa kama kuna changamoto ya kutosikilizwa basi wanapaswa kurudi tena kwenye ofisi yake ili watafutiwe njia mbadala ya kujibiwa kero hizo.

 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.