Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai amesema chanjo ya ugonjwa wa homa ya sotoka ni mkombozi kwa wafugaji wa Kongwa ambao wametaabika kwa muda mrefu.
Pia, Ndugai amewataka wataalamu kwenda mbele zaidi kwa kuanza kutazama uwezekano wa kutengeneza chanjo ya Ukimwi ili wananchi wafurahie maisha.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ndugai kuonekana hadharani tangu alipojiuzulu nafasi ya Spika wa Bunge Januari 6 mwaka huu, huku wengi wakitaka kujua aliko baada ya kutoonekana bungeni.
Ndugai ameonekana hadharani jana Jumatatu Aprili 11, 2022 katika uzinduzi wa chanjo ya mifugo ya ugonjwa wa homa ya sotoka uliofanyika katika Wilaya ya Kongwa.
Akizungumza mbele ya wafugaji katika uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, Ndugai amesema kwa watu wa Kongwa ni furaha na neema ambayo wanapaswa kuishukuru Serikali ya awamu ya sita.
Spika huyo wa zamani amesema kwa namna yoyote ufugaji wa mbuzi ulishashindikana katika wilaya hiyo lakini uwepo wa chanjo unakwenda kuwainua wafugaji akiwemo yeye kuwekeza zaidi kwenye mbuzi.
"Nampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kutukumbuka watu wa Kongwa, Mheshimiwa Waziri tupelekee salamu na pongezi nyingi sana,"amesema Ndugai.
Katika hatua nyingine ameahidi kufanya kazi na kushauriana na Waziri Ndaki kwani amepangwa katika kamati ya Kilimo Mifugo na Maji ambayo ipo chini ya Wizara hiyo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.