ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 22, 2022

Benki ya CRDB yafuturisha wateja wake jijini Mwanza, yatoa zawadi kwa watoto

 

Benki ya CRDB imewafuturisha wateja wake jijini Mwanza ikiwa ni mwendelezo wa utamaduni wa benki hiyo kuungana na waumini wa dini ya Kiislamu wanaoishiriki mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Hafla ya Iftar hiyo imefanyika Alhamisi Aprili 21, 2022 katika ukumbi wa Gold Crest mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya Ilemela Hassan Masala na kuhudhuriwa pia na viongozi mbalimbali akiwemo Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza Hassan Kabeke.

Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta alisema benki hiyo imekuwa na desturi ya kujumuika pamoja na wateja wake katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kupata Futari ya pamoja na kuimarisha mahusiano miongoni mwa pande zote mbili.

Sitta alitumia fursa hiyo waeleza waumini wa dini ya Kiislamu kwamba benki ya CRDB imeanzisha huduma ya Al-Barakah Banking inayoendana na misingi ya dini hiyo ikiwa ni pamoja na mikopo isiyo na riba na hivyo kuwaepusha kuingia kwenye dhambi ya riba.

Mkuu wa Huduma ya Al-Barakah Banking (Islamic Banking), Rashid Rashid alisema uanzishwaji wa huduma hiyo unadhihirisha kauli mbiu ya namna benki ya CRDB isemayo 'Benki Inayomsikiliza Mteja' ambapo kupitia maoni ya wateja wake iliamua kuanzisha huduma ya Al-Barakah.

Rashid aliongeza kuwa akaunti zinazofunguliwa kupitia huduma ya Al- Barakah zina uangalizi maalum unaohakikisha hazitumiki kwenye miamala inayokinzana na maadili ya imani ya kiislamu ikiwemo riba na kuwaondolea changamoto iliyokuwepo zamani ya kuhifadhi fedha kwenye mabenki yanayokinzana na misingi ya sharia.

Naye Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke aliishukuru benki ya CRDB kwa kuwaondolea waislamu na wasio waslamu dhambi ya kuingia kwenye riba baada ya kuanzisha huduma ya Al- Barakah kwani riba ni dhurma kubwa na watu wengi wamefirisika kutokana na kuingia kwenye dhambi hiyo, akisema "yeyote anayeingia kwenye riba ajiandae kupigana vita na Mwenyezi Mungu, CRDB wametutoa huko".

Sheikh Kabeke aliagiza misikiti, Kata na Wilaya zote za Mkoa Mwanza kutii maelekezo ya Mufti wa Tanzania ya kutaka akaunti zote za BAKWATA nchini kufunguliwa ndani ya huduma ya Al- Barakah. "Tumeanzisha mchakato wa kujenga Vituo vya Afya katika Wilaya zote saba za Mkoa Mwanza, akaunti ambayo tumewaomba waislamu na wasiokuwa waislamu wachangie humo michango yao ni akaunti ya Al-Barakah" alisema Sheikh Kabeke.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Ilemela, Hassan Masala alisema Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na benki ya CRDB katika kuwahudumia watanzania kupitia huduma zake zenye ubunifu ikiwemo Al-Baraka Banking inayowapa wasilamu huduma zinazotimiza matakwa ya dini yao.

"Tunatambua kazi kubwa mnayoifanya, miradi yetu mingi, fedha zetu nyingi na biashara kubwa, Serikali inafanya na benki ya CRDB, lakini mmeanzisha huduma ambazo zinagusa makundi mbalimbali kama hii ya Al-Barakah, kwa kweli tunaiona nia yenu njema" alisema Masala wakati akizungumza kwenye Iftar hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Meneja wa benki ya CRDB Kanda ya Ziwa akizungumza kwenye Iftar hiyo.
Meneja wa benki ya CRDB akizungumza kwenye Iftar iliyofanyika jijini Mwanza.
Mkuu wa Matawi Benki ya CRDB, Boniventure Paul alisema katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, lisha ya benki hiyo kujumuika pamoja na wateja wake kwenye futari pia hutoa msaada vyakula/ futari kwenye vituo vya kulelea watoto vyenye uhitaji mkubwa ili kuwawezesha watoto na walezi wao kutekeza vyema ibada ya swaum.
Mkuu wa Islamic Banking (Al-Barakah), Rashid Rashid akizungumza kwenye hafla hiyo.
Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke akizungumza kwenye Iftar hiyo.
Mkuu wa Wilaya Ilemela, Hassan Masala akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya Ilemela, Hassan Masala akizungumza kwenye Iftar hiyo ambayo aliwahimiza pia waislamu kuendelea kutenda matendo mema, kuswali na kujinyenyekeza mbele za Mwenyezi Mungu nyakati zote na si wakati wa Mwezi Mtukufu tu.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akipata riziki ya Iftar iliyoandaliwa na benki ya CRDB jijini Mwanza.
Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke akiwa kwenye Iftar hiyo.
Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Kanda Bugando, Dkt. Fabian Massaga akichukua riziki kwenye Iftar hiyo akiwa ameambatana na wateja mbalimbali wa benki ya CRDB.
Wateja wa benki ya CRDB jijini Mwanza wakipata riziki ya Iftar.
Wateja wa benki ya CRDB jijini Mwanza wakiwa kwenye hafla hiyo.
Viongozi mbalimbali akiwemo Sheikh wa BAKWATA Mkoa Mwanza Hassan Kabeke (katikati) wakipata Iftar iliyoandaliwa na benki ya CRDB jijini Mwanza.
Wateja na wafanyakazi wa benki ya CRDB wakiwa kwenye Iftar hiyo.
Uongozi wa benki ya CRDB umetumia fursa hiyo pia kukabidhi zawadi ya bidhaa mbalimbali za vyakula kwa ajili ya watoto wanaolelewa katika Vituo mbalimbali jijini Mwanza.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.