Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu wa nne kutoka kushoto akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kamati ya utendaji ya APC pamoja na wafanyakazi wake |
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akisaini kitabu cha wageni alipotembelea ofisi za chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Arusha (APC) |
Na Seif Mangwangi, Arusha
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amepongeza uongozi wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha (APC), kwa ushiriki wake katika maendeleo ya uhifadhi nchini ikiwemo mapambano dhidi ya ujangili na uhamasishaji utalii wa ndani.
Kanyasu ameyasema hayo wakati akizungumza na uongozi wa Kamati ya utendaji ya APC alipofanya ziara katika ofisi hizo kwa lengo la kujionea shughuli ambazo zimekuwa zikifanywa na klabu hiyo na kusikiliza changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo.
Amesema Mkoa wa Arusha ni kitivo kikuu cha utalii na wakati wote ambapo amekuwa akifuatilia taarifa za utalii waandishi wa habari wa Arusha wamekuwa wakiongoza kuandika taarifa hizo ambazo matokeo yake yamekuwa makubwa kwa jamii.
“Arusha mmekuwa na mchango mkubwa sana kwenye suala la maendeleo ya utalii nchini, ukizungumzia ujangili ambao umeshuka kwa asilimia kubwa sana nchini mchango wenu ni mkubwa sana, kwa kweli kama Wizara tunawapongeza sana,”anasema.
Anasema Wizara yake itaendelea kushirikiana na waandishi wa Arusha na wengine wote nchini ili kuendelea kuhamasisha utalii wa ndani pamoja na mapambano dhidi ya ujangili unaofanywa na watu wachache wenye nia mbaya ovu kwa nchi ya Tanzania.
Awali Mwenyekiti wa APC, Claud Gwandu, alimweleza Naibu Waziri kuwa waandishi wa habari wa Arusha wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na uongozi wa Mamlaka ya hifadhi za Taifa (TANAPA), katika kutangaza shughuli za utalii.
Amemweleza Naibu Waziri kuwa hivi sasa APC iko kwenye maandalizi ya kuandaa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, yanayoadhimishwa Mei 3 ya kila mwaka ambapo inatarajia kukutanisha waandishi wote wa Arusha na kujadili changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo mwaka mzima.
Amesema katika maadhimisho hayo APC inatarajia kuzindua televisheni yake (APC Online tv), zpamoja na blogu ambazo mbali ya kutumika kuuhabarisha umma masuala ya kijamii pia zitakuwa na vipindi maalum vya kutangaza utalii.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.