ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, November 25, 2019

VIJANA WANAOGOPA ZAIDI MIMBA KULIKO UKIMWI


NA ALBERT SENGO / GSENGOTv

Maambukizi mapya ya VVU bado yanatokea nchini. Takwimu zinaonyesha kuwa watu takribani 72,000 hupata maambukizi mapya nchini; hii ni sawa na wastani wa watu 6,000 kwa mwezi ama watu 200 kwa siku au watu 8 kwa saa. 
 Akimwakilisha Waziri wa Afya Dr. Ummy Mwalimu, mgeni rasmi wa Uzinduzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani ambapo kilele chake kitakuwa Tarehe mosi Disemba, Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella amesema kutokana na  asili ya shughuli zinazofanyika, biashara na muingiliano wa idadi kubwa wa watu wanaoingia na kutoka, maeneo ya visiwa vya mkoa wa Mwanza yanatajwa kuwa sehemu hatarishi.

Aidha Unyanyapaa unatajwa kuwa tishio kubwa kuliko VVU na UKIMWI. Kama inavyojulikana mapambano ya Virusi vya Ukimwi huanzia pale mtu anapoitambua afya yake, Bi. Leticia Moris ni mwenyekiti wa baraza la watu wanaoishi na vurusi vya UKIMWI anasema Pamoja na watu kujitokeza kwa wingi katika mazoezi mbalimbali ya upimaji VVU, idadi kubwa ya watu wanashindwa kufuata dozi au kuendelea na dozi kwa kuhofia kuonwa na watu na kunyooshewa vidole, hivyo wamekuwa watoro wa dawa.

 "Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu wa 2019 ni “JAMII NI CHACHU YA MABADILIKO; TUUNGANE KUPUNGUZA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU” Hivyo, msisitizo mkubwa katika Kauli Mbiu ya mwaka huu ni ushiriki wa jamii kwenye  kupunguza maambukizi mapya ya VVU kuanzia kwenye kuibua changamoto, kupanga mipango utekelezaji wa mipango na tathmini ya mipango hiyo.
Imefahamika kuwa ushirikishwaji wa jamii una tija kubwa unapofanywa kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji ya mahali husika. Jamii ndio yenye uwezo mkubwa wa ushawishi kwa mtu mmoja mmoja, familia na hata kwa viongozi wanaowawakilisha. 
Aidha, kauli mbiu hii inatilia mkazo kwenye kuunganisha nguvu katika kupunguza maambukizi mapya ya VVU na hasa kwenye kundi la vijana. 
Takwimu zinaonyesha kuwa kundi la vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 linachangia maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 40 na hivyo kulifanya kundi hili kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya VVU kuliko kundi lingine.
 "Vijana wa umri huu hofu yao kubwa siyo UKIMWI, siyo Magonjwa ya zinaa bali wanaogopa MIMBA" Amesema Bw. Yassin Ally ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la kupambana na Ukatili wa Jinsia, Utetezi wa Wanawake na Watoto (KIVULINI) na kisha kuongeza.
"Kwa hiyo utaona msisitizo mkubwa wengi wanadiriki mpaka kujifungia njiti mashuleni au nje ya shule wakikwepa mimba, ni lazma tutafakari tunabadilishaje mbinu ili kuokoa kizazi chetu" 

Hivyo Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha Wananchi, Makampuni na makundi mbalimbali ya jamii kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kudhibiti VVU/UKIMWI nchini ili kwa pamoja tuweze kuendana na mtazamo wa kimataifa wa kumaliza maambukizi mapya ya VVU ifikapo mwaka 2030.







 









Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.