ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, July 17, 2019

TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI YASEMA MKAKATI WA SERIKALI NI KUENDELEZA KILIMO CHA UMWAGILIAJI



Na Ripota,Michuzi TV-Morogoro

TUME ya Taifa ya Umwagiliaji imesema kuwa mpango mkakati wa Serikali ni kuendeleza kilimo cha umwagiliaji nchini.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Marco Ndonde akiwa wilayani Mvomero mkoani Morogoro ambako yeye,Wataalamu  na maofisa wengine wamekwenda kuangalia shughuli za kilimo cha umwagiliaji zinazofanyika katika Shamba la Skimu za Umwagiliaji Dakawa,Mvomero mkoani Morogoro, ambayo miundombinu yake imeboreshwa kupitia ufadhili wa fedha wa Serikali ya Marekani.

Hivyo amefafanua kuwa mpango kazi ambao umefanyiwa mapitio mwaka 2018 ni kwamba Serikali imejipanga kufanya kilimo cha umwagiliaji kwa kutotegemea mvua, kwa kuwa na miundombonu ya maji hasa kwa kuvuna maji kupitia mabwawa.

"Hivyo katika mpango kazi tumepanga kujenga mabwawa kwa awamu mbili 
awamu ya kwanza ni kuanzia mwaka 2018- 2025 mabwawa 51 na awamu ya 2026 hadi mwaka 2035.

"Kwa ujumla wake tunatarajia kujenga na kukarabati jumla ya mabwawa 112 na kwa kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2035 na lengo ni kuwa na skimu za umwagiliaji ambazo zinapata maji kwa muda wote na zinakuwa zinavuna maji kupitia mabwawa ambayo yatakuwa yamejengwa,"amesema.

Ameeleza kazi zote za ujenzi wa miundombinu na ukarabati wa skimu ni fedha ambazo zimetoka Serikali ya Marekani na kwamba jumla ya Sh.bilioni 24 zimetumika ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu , kuweka pampu na kusakafia mifireji.

"Nitoe shukrani kwa Serikali ya Marekani kwani kupitia ufadhili wao tumeweza kuboresha miundombinu kwenye skimu hii na leo hii faida yake tunaiona.

"Huko nyuma tulikuwa tunaboresha skimu juu juu tu lakini hivi sasa tumeziboresha kwa kiwango kikubwa sana,"amesema Ndonde na kueleza kuwa Serikali kupitia JICA kuna mradi wa kusaidia wakulima wadogo, ambao huo nao utawezesha kukamilika kwa skimu nyingine na mkakati uliopo ni kuhakikisha skimu zote zinakuwa na miundombinu iliyoboreshwa.

Ndonde amesema na ili kufikia hatua hiyo ni vema wakawa wanatengeneza miundombinu kwa skimu chache chache badala ya kufanya katika skimu nyingi kwa wakati mmoja.

Hata hivyo amesema kuna sera ya Taifa ya umwagiliaji inayoshauri na kueleza kuwa mifereji mikuu yote isakafiwe , hivyo wanakwenda na sera hiyo.
 Mfereji mkubwa wa kusambaza maji katika mashamba ya Mpunga,ukiwa umesakafiwa vizuri kuhakikisha maji yanayotumika kumwagilia mashamba hayo hayapotei tena,kufuatia ukarabati mkubwa kufanywa katika miundo mbinu ya Skimu za Umwagiliaji  ndani ya mashamba hayo.
Moja ya Shamba la Mpunga.

   Mwenyekiti wa Ushirika Wakulima Wadogowadogo  Kilimo cha Umwagiliaji Mpunga Dakawa,Mvomero mkoani Morogoro Bwa.Thomas Kakema  akimuonesha Kaimu Mkurugenzi Tume ya Taifa ya  Umwagiliaji Bwa.Marco Ndonde namna Miundombinu ya Skimu za Umwagiliaji zilivyoboreshwa katika shamba hilo la Ushirika.
 Pichani wa pili kulia,Kaimu Mkurugenzi Tume ya  Taifa ya Umwagiliaji Bwa.Marco Ndonde akimsikiliza Mwenyekiti wa Ushirika Wakulima Wadogowadogo  Kilimo cha Umwagiliaji Mpunga Dakawa,Mvomero mkoani Morogoro Bwa.Thomas Kakema alipokuwa akimuonesha namna Miundombinu ya Skimu za Umwagiliaji zilivyoboreshwa katika shamba hilo la Ushirika.
 Sehemu ya mashine za kusukuma maji na kupeleka kwenye mashamba ya Mpunga kupitia mifereji ambayo kwa sasa imekarabatiwa na kuwa bora zaidi,kuhakikisha maji hayapotei 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.