ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, June 17, 2019

KIWOHEDE, AGAPE WAUNGANA NA SERIKALI YA MKOA WA SHINYANGA KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA


Na Marco Maduhu - Malunde1 blog Kahama. Mashirika yasiyo ya kiserikali KIWOHEDE na AGAPE ACP, ambayo yanatekeleza miradi ya kupinga matukio ya ukatili dhidi ya watoto wadogo pamoja na kutokomeza mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga, yameungana na Serikali ya mkoa wa Shinyanga kuadhimisha kilele cha siku ya mtoto wa Afrika.
Maadhimisho ya kilele ya Siku ya Mtoto wa Afrika yamefanyika leo Juni 16, 2019 katika mkoa wa Shinyanga yamefanyika kwenye uwanja wa michezo wa taifa wilayani Kahama ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Kahama, Mhe. Anamringi Macha, akimwakilisha mkuu wa mkoa,Mhe. Zainab Telack. Mhe. Macha aliitaka jamii kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambapo aliwasisitiza wazazi kuacha tabia ya kuwafanyia vitendo vya kikatili watoto wao pamoja na kuwabagua kuwapatia elimu na kufikia hatua ya kuwaozesha ndoa za utotoni wanafunzi wa kike. Alisema serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayekamatwa akiwafanyia ukatili watoto. Mhe. Macha alitumia fursa hiyo kuyapongeza mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani humo likiwemo KIWOHEDE na AGAPE, kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kushirikiana na serikali kutatua changamoto mbalimbali ndani ya jamii. Naye Mratibu wa mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi, Ujinsia na haki kwa vijana  wa Shirika la KIWOHEDE,Amos Juma aliitaka jamii kuachana na vitendo vya kunyanyasa watoto wao pamoja na kuacha tabia ya kuendekeza mila na desturi kandamizi kwa kuwaozesha watoto na hatimaye kuzima ndoto zao. Alisema katika mradi wao wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia na kutetea haki za vijana, ambao wanautekeleza kwenye kata ya Zongomela, wamekuwa wakikumbana na changamoto ya jamii kupenda kuendekeza mila na desturi zilizopitwa na wakati, na hivyo kuwapatia changamoto kubwa ya kumaliza kabisa ukatili kwa watoto licha ya kuupunguza kwa asilimia kubwa.
KIWOHDE kama wadau wakubwa wa kutetea haki za watoto, tunapenda kutumia fursa hii kwenye maadhimisho haya ya siku ya mtoto wa Afrika Duniani, kuwataka wazazi waachane na mila kandamizi pamoja na kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto wao, bali wawatekelezee mahitaji hayo pamoja na kuwapatia elimu bila ya kuwabagua ili wapate kutimiza ndoto zao,”alisema Juma. “Mradi huu tulianza kuutekeleza mwaka 2017 na unatarajiwa kuisha mwaka huu 2019, ambapo kipindi tunauanza kuutekeleza kwenye Kata ya Zongomela, kulikuwa na matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto zikiwamo na mimba za wanafunzi, lakini kwa sasa matukio hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa tofauti na awali,”aliongeza. Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto kutoka Shirika la AGAPE mkoani Shinyanga, Felix Ngaiza, ambao wanautekeleza wilayani Kishapu katika kata za Itilima, Kishapu na Bunambiu, aliitaka jamii kuachana na vitendo vya kikatili pamoja na kuwaozesha wanafunzi ndoa za utotoni. Ngaiza alisema AGAPE itaendelea kushirikiana na serikali na jamii ili kuhakikisha watoto na wanawake wanapata haki kwa wakati katika jamii. Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika mwaka 2019  inasema “ Mtoto ni Msingi wa Taifa Endelevu, Tumtunze, Tumlinde na Kumwendeleza.” TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI Mkuu wa wilaya ya Kaham,Mhe. Anamringi Macha akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo katika mkoa wa Shinyanga yamefanyika katika uwanja wa michezo wa taifa Mjini Kahama leo Juni 16,2019Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog
Awali vijana kutoka Shirika la KIWOHEDE wakiongoza maandamano ya wanafunzi kutoka katika halmashauri ya Kahama Mji kuelekea kwenye uwanja wa taifa wilayani Kahama kwa ajili ya kuadhimisha kilele siku ya mtoto wa Afrika kimkoa wilayani Kahama.
Wanafunzi wakiwa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kimkoa wilayani Kahama. Watoto wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika. Wanafunzi wakiwa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kimkoa wilayani Kahama. Awali mkuu huyo wa wilaya ya Kahama Kabla ya kutoa hotuba yake kwenye maadhimisho hayo ya siku ya mtoto wa Afrika, alitembelea mabanda ya wadau wa maendeleo. Pichani ni Mhe. Macha akiwa kwenye banda la Shirika la KIWOHEDE akisikiliza kazi ambazo wanazifanya za kutetea haki za watoto pamoja na kuwapatia vijana mafunzo ya ujasiriamali. Mkuu wa wilaya ya Kahama,Mhe. Anamringi Macha, akiangalia nguo za batiki ambazo hutengenezwa na vijana wa kike kutoka Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama. Kulia ni Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi, Ujinsia na Haki kwa Vijana  wa Shirika la KIWOHEDE,Amos Juma akimwelezea mkuu wa wilaya ya Kahama,Mhe. Anamringi Macha namna wanavyofanya kazi wilayani humo ya kutatua changamoto mbalimbali ndani ya jamii ikiwamo kutokomeza mimba na ndoa za utotoni. Mratibu wa mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi, Ujinsia na haki kwa vijana  wa Shirika la KIWOHEDE,Amos Juma  akieleza namna shirika hilo linavyowasaidia vijana wa kike kwa kuwajengea uwezo wa kufanya shughuli za ujasiriamali ikiwamo kutengeneza batiki, na kushona nguo. Mkuu wa wilaya ya Kahama,Mhe. Anamringi Macha akiwa kwenye banda la Shirika la AGAPE, akisikiliza kazi ambazo wanazifanya za kutetea haki za wanawake, watoto kwa kupinga matukio ya ukatili pamoja na kutokomeza mimba na ndoa za utotoni. Msimamizi wa mradi wa Sauti ya mwanamke na mtoto kutoka Shirika la AGAPE ,Felix Ngaiza, akimwelezea mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Anamringi Macha namna mradi huo unavyofanya kazi, ambao umelenga kutokomeza matukio ya ukatili pamoja na mimba na ndoa za utotoni na kubaki kuwa historia, ambapo mradi huo unatekelezwa wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga. Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akiwa kwenye banda la Shirika la TVMC, akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa miradi Adriana Leonard namna shirika hilo linavyofanya kazi. Vijana kutoka Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama wakitoa burudani kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto Afrika kimkoa wilayani Kahama. Wanafunzi kutoka Compassion wilayani Kahama nao wakitoa burudani kwenye kilele cha maadhimisho hayo ya siku ya mtoto wa Afrika kimkoa wilayani Kahama. Wanafunzi kutoka shule ya Sekondari Mwendakulima wilayani Kahama nao wakitoa burudani kwenye kilele cha maadhimisho hayo ya siku ya mtoto wa Afrika kimkoa wilayani Kahama.
Vijana kutoka Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama wakipiga picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kuadhimisha kilele cha siku ya mtoto wa Afrika kimkoa wilayani Kahama. Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.