ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, March 21, 2019

WANAFUNZI WALIOCHORA PICHA YA KUMDHIHAKI RAIS WA BURUNDI WASHITAKIWA.

Wanafunzi waliochora picha ya kumdhihaki Rais wa Burundi washitakiwa

Wanafunzi watatu wa kike wamefunguliwa mashitaka ya kumdhihaki Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, na huenda wakahukumiwa kifungo cha hadi miaka mitano jela.
Msemaji wa Mahakama ya Juu ya Burundi, Agnès Bangiricenge amesema leo Alkhamisi kuwa, wanafunzi hao wameshitakiwa kwa kumdhalilisha rais wa nchi, kwa kuchora picha yake na kisha kuichafua kwa kuipaka rangi.
Wanafunzi hao walikamatwa juma lililopita kwa kosa la kuchora na kupaka rangi picha ya Rais Nkurunziza katika vitabu vyao vya shule, kitendo ambacho vyombo vya mahakama vinasema ni kuidhihaki na kuidhalilisha shakhsia ya rais, ambaye ni nembo ya umoja wa kitaifa.
Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema wanafunzi saba walikamatwa wakihusishwa na kitendo hicho, lakini wanne wakaachiwa huru.

Burundi imekuwa ikituhumiwa na UN kuwa inakiuka haki za binadamu

David Ninganza, mtetezi wa haki za watoto nchini humo amesema ingawaje ni kinyume cha sheria kumvunjia heshima kiongozi wa nchi kwa namna yoyote ile, lakini kwa kuwa kosa hilo (la kuchora na kupaka rangi picha ya rais) limefanywa na wanafunzi, hawakupaswa kufunguliwa mashitaka kwa kuwa kitendo hicho hakikuwa cha kisiasa.
Mwaka 2016, watoto 11 walifungwa jela kwa tuhuma za kuchora vibonzo vya kumdhalilisha Rais Nkurunziza katika vitabu vyao vya shule. Mwaka huohuo, wanafunzi wengine 300 walifukuzwa shule baada ya kuchora picha za kumdhihaki rais.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.