ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, November 6, 2018

MAMA AMUUA MWANAE KWA KIPIGO AKIMTUHUMU KUIBA MAEMBE KWA JIRANI, AMTUNDIKA DARINI ILI KUPOTEZA USHAHIDI AKISEMA AMEJINYONGA.


GSENGOtV

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunamshikilia mwanamke mmoja aitwaye RAHEL MATALAKA, miaka 41, mkazi wa kijiji cha lugenge, kwa tuhuma za kumpiga hadi kumuua mtoto wake wa kiume aitwaye MALIATABU CONSTANTINE, miaka 10, mwanafunza wa darasa la pili shule ya msingi Ikeleg,Wilayani Misungwi.

Tukio hilo la mauaji limetokea tarehe 03.11.2018 majira ya 19:00hrs usiku, hii ni baada ya mama wa marehemu kuletewa malalamiko kuwa mtoto wake alikua akiangusha na kuiba maembe kwa jirani. Ndipo mtuhumiwa alipatwa na hasira na kumpiga mtoto kwa kutumia fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyopelekea mtoto kupoteza fahamu na baadae kufariki dunia.

Mtuhumiwa alipoona mtoto amepoteza maisha alimchukua na kumtundika juu ya mwembe kwa kutumia kipande cha khanga ili apoteze ushahidi ili baadae ionekane kuwa amejinyonga. Ndipo majirani walipoona tukio hilo walitoa taarifa kituo cha Polisi.  Aidha baada ya polisi kupata taarifa hizo tulifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.

Polisi tunaendelea na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani. Mwili wa marehemu tayari umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa  ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

Katika tukio la pili, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tumefanikiwa kukamata gari moja lililoibiwa lenye namba T.233 CDG aina ya Toyota Carina mali ya RENATUS ELIUS, mkazi wa mtaa wa Ghana, likiwa limetelekezwa kando ya barabara huko maeneo ya Kitangiri Wilayani Ilemela.

Gari hilo liliibiwa tarehe 01.11.2018, ndipo mmiliki wa gari alitoa taarifa polisi juu ya kuibiwa kwa gari lake. Polisi baada ya kupata taarifa hizo tulifanya msako mkali kwa kushirikisha vikosi vyetu vya askari wa kufuatilia wezi wa magari na Intelejensia. Ndipo tarehe 04.11.2018 majira ya mchana tulifanikiwa kulikamata gari hilo likiwa limetelekezwa kando ya barabara huko mtaa wa kitangiri huku wezi wakiwa wametoroka.

Aidha baada ya kulikamata gari hilo, tulilifanyia ukaguzi na kugundua baadhi ya vifaa vya gari hilo vimetolewa ambavyo ni betrii ya gari moja, tairi  ya gari moja, jeki moja, radio ya gari, power window na show ya mbele ya gari. Polisi tunaendelea na msako mkali wa kuhakikisha wezi hao wanapatikana.

Katika tukio la tatu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunamshikilia mwanamke mmoja aitwaye MALAGALITA MATHIAS, miaka 55, mkazi wa kijiji cha Nyatukala, kwa kosa la kupatikana na pombe ya moshi (gongo) kiasi cha lita 20 na dawa za kulevya aina ya mirungi kiasi cha kilo moja, huko maene ya kijiji cha Nyatukala Wilayani Sengerema.

Tukio hilo limetokea tarehe 05/11/2018 majira ya 17:00hrs jioni, hii ni baada ya kupatikana kwa taarifa kwamba katika Vijiji vya Nyamizeze na Nyatukala vilivyopo Wilayani Sengerema wapo watu wanaojihusisha na uuzaji pamoja na utengenezaji wa pombe ya gongo na dawa za kulevya aina ya mirungi.

Aidha baada ya kupatikana kwa taarifa hizo Polisi tulifanya msako mkali katika vijiji hivyo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa tajwa hapo juu akiwa na kiasi hicho cha pombe ya moshi na mirungi huku wenzake wakifanikiwa kutoroka.

Polisi tunaendelea na mahojiano na mtuhumiwa ili kuweza kubaini wenzake anaoshirikiana nao katika biashara hiyo haramu ya gongo na mirungu, pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Katika tukio la nne, mtoto mmoja wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa siku 2 hadi 3 ameokotwa akiwa hai baada ya kutupwa kichakani kandokando mwa ziwa Victoria na mtu asiyefahamika, huko maeneo ya Bwiru ziwani Wilayani Ilemela.

Tukio hilo limetokea tarehe 01.11.2018 majira ya 14:00hrs, hii ni baada ya watu waliokua wakipita njiani kusikia sauti ya mtoto akilia toka kichakani ndipo walifuatilia na walipoona ni mtoto walitoa taatifa polisi.

Polisi tulifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio na kukuta mtoto wa kike akiwa ametupwa kichakani hapo akiwa hai huku mwiliwake ukiwa umeviringishwa kwenye mfuko wa sandarusi.

Mtoto amepata matibabu na hali yake inaendelea vizuri amekabidhiwa katika shirika la Forever Angel lililopo Bwiru Wilayani  Ilemela  kwa ajili ya hifadhi. Polisi tunaendelea na upelelezi pamoja  na msako mkali wa kumtafuta mama wa mtoto huyo.

Katika tukio la tano; Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunamshikilia tapeli/mwizi mmoja aliyefahamika kwa jina la BENEDICTO BAHATI, miaka 29, mkazi wa kiloleli, kwa tuhuma za kujifanya afisa wa TCRA, kitendo ambacho ni kosa la jinai.

Tukio hilo limetokea tarehe 02.11.2018, majira ya 16:30hrs, hii ni baada ya mtuhumiwa kwenda kwa mtumishi wa benki ya CRDB tawi la Nyegezi -Malimbe na kumtapeli kuwa yeye ni afisa wa TCRA Mkoa wa Mwanza, hivyo amefika hapo akidai anazo taarifa zake ambazo zinaonesha amekuwa akifanya mawasiliano yasiyo rasmi.

 Hivyo ametumwa na ofisi ya TCRA Mwanza kufuatilia taarifa hizo, na kumtaka atoe fedha kiasi cha laki tano ili aweze kumfichia siri ili asitoe taarifa hizo kwa mamlaka inayohusika yaani TCRA.

Baada ya hapo mlalamikaji alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambapo Polisi tulituma askari makachero na wamakosa ya mtandao na badae tulifanikiwa kumtia tapeli huyo nguvuni. Polisi tunaendelea na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.Aidha msako mkali wa kuwatafuta wenzeka anaoshirikiana nao katika uhalifu huo bado unaendelea.

Tukio la sita, Mafanikio ya misako Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tumefanikiwa kukamata gari moja aina ya IST rangi ya Silver lenye namba T.892 DFY/DKY na pikipiki mbili moja inanamba MC.836 ASK aina ya BOXER na nyingine aina ya FEKON lakini haina namba. Gari na pikipiki hizo zimekamatwa baada ya kutumika katika matukio ya kiuhalifu katika maeneo mbalimbali ya Jiji na Mkoa wa Mwanza.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa wakazi wa Jiji na Mkoa wa Mwanza tukiwataka waache vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, pindi mtoto anapokosea apewe  kalipio na akanywe na kuonyeshwa madhara ya wizi ili atambue kosa na wala sio vipigo. Sambamba na hilo tunawataka vijana waache tabia ya kujihusisha na uhalifu kwani utawagharimu.

Imetolewa na:
Jonathan Shanna – ACP
Kamanda wa Polisi (M) Mwanza
06 November, 2018.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.