Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe.SHANIF MANSOOR, amekabidhi kiasi cha shilingi milioni 4 kwa ajili ya kukarabati na kuboresha miundombinu ya Shule ya Sekondari Ngudu iliyopo wilayani humo.
Akipokea mchango huo wakati wa mahafali ya 2 ya kidato cha 4 Mwenyekiti wa shule hiyo, FEISALL YASIN, amempongeza mbunge huyo, kwa namna ambavyo amekuwa akijitolea katika masuala mbalimbali ya maendeleo, na sasa amerudi tena kuikwamua shule hiyo ili vijana wanaosoma shuleni hapo wapate nafasi ya kutimiza ndoto zao.
"Kama kumbukumbu zangu ziko sahihi nakumbuka Mhe. MANSOOR, alitumia zaidi ya shilingi milioni 100 toka kwenye mshahara wake, wakati akiwa diwani wa kata yetu ya Ngudu kuhakikisha swala la elimu linasonga mbele. Hii leo amerudi tena, huu ni moyo wa kizalendo na wakipekee" alisema FEISAL na kisha akaongeza.
"Shule nyingi vijijini zina vijana wengi wenye akili na wabunifu lakini wanakwamishwa na changamoto zilizopo kwenye shule zetu, kama vile ukosefu wa maabara na vitendea kazi vyake, vitabu vya kutosha, miundombinu ya kutosha yakiwemo majengo ya ofisi za waalimu na madarasa, uchache wa shule za sekondari ni chanzo cha kushindwa kupata matokeo mazuri ambapo husababisha wanafunzi wetu kusafiri umbali mrefu na kufika shuleni wakiwa wameshachoka"
Licha ya kuipongeza Serikali ya awamu ya tano ya Mhe. Dkt. JOHN POMBE MAGUFULI, kwa kutoa elimu bila malipo, Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe. SHANIF MANSOOR, amesema ni kwa kipindi kirefu amekuwa na ndoto ya kuona jimbo lake likifanya vyema katika utoaji wa elimu na ufaulu na hata baadaye kuwa mfano wa kuigwa sanjari na kugeuka kuwa kimbilio kwa wazazi wa wilaya na mikoa mbalimbali nchini linapokuja suala la elimu.
Katika kukuza michezo shuleni hapo Mbunge huyo amewapatia mipira 8, pamoja na kuwajengea magoli katika uwanja wao wa soka.
Kwa upande wake Katibu tawala wa wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, NIKIA ALLY, amewataka wazazi kuacha mara moja kuoza watoto kwani ni moja ya vyanzo vinavyo warudisha nyuma kimaendeleo na kuchangia umasikini, akisisitiza kuwa hato muonea haya yule yeyote atakaye kutwa na hatia ya kujihusisha au kushiriki kufanikisha vitendo hivyo.
Zaidi ya wanafunzi 50 wilayani Kwimba mkoani Mwanza, wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na mimba zisizo tarajiwa.
Pamoja na kufanya vizuri katika masomo ya sayansi, shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa waalimu kumi wa somo la Sayansi.
Shule ya Sekondari Ngudu inazaidi ya wanafunzi 1100 huku wanafunzi 400 wakiishi bweni.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.