ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, September 18, 2018

MWANDISHI WA HABARI MMOJA ANAUAWA DUNIANI KILA BAADA YA SIKU 5



GSENGOtV
TAKWIMU zinaonyesha kwamba duniani mwandishi mmoja anauawa kila baada ya siku 5, katika harakati za kutekeleza majukumu yake ya uandishi.
Tume ya Taifa ya Unesco imesema waandishi wa habari 73 wamepoteza maisha kwa miaka miwili iliyopita kwenye nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wakati wakitekeleza majukumu yao.
Dokta Moshi Kimizi (kulia) akiwasilisha taarifa, Naibu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Warioba Sanya (katikati) na Dr. Eva Solomon Msangi toka SJMC-UDSM.
Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Dokta Moshi Kimizi amesema taarifa ya ufuatiliaji ya Unesco inaonyesha waandishi walivyotishwa na kunyamazishwa wakati walipoeleza ukweli juu ya mambo mbalimbali yaliyoizunguka jamii.
Katika hotuba yake wakati wa kufungua semina kwa waandishi wa habari wa kanda ya ziwa leo Septemba,18,2018 kuhusu jinsi ya kuzikabili changamoto za usalama amesema kwa miaka kumi iliyopita waandishi 820 wamepoteza maisha duniani kote.
Amesema waandishi wa habari wanatakiwa kuzingatia mbinu mbalimbali kwa ajili ya usalama wao wakati wa kutekeleza majukumu yao huku wakiwajibika kufanya kazi kwa ufanisi.
Ameongeza Tume hiyo pamoja na kuhakikisha unakuwepo uhuru wa habari na usalama wa waandishi wa habari pia wanafuatilia shughuli zote zinazofanywa na Unesco hapa nchini zenye tija kwa Taifa.
Warioba Sanya.
 Kwa upande wake, Naibu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza aliyekuwa mgeni rasmi Warioba Sanya amesema Serikali imeendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa waandishi wa habari na hakuna kitisho kikubwa kwa sasa.
Amesema pamoja na kutokuwa na matukio ya kuuawa kwa waandishi wa habari wakati wa kutekeleza majukumu yao waandishi wanatakiwa kujiandaa kiusalama kwa ajili ya miaka ijayo.
"Hapa nchini hatujawa na matukio ya kuuawa kwa waandishi wa habari, sisi hatujafika huko lakini huwezi kujua mazingira ya baadaye Serikali inawahakikishia usalama muda wote msishindwe kutekeleza majukumu yenu" amesema Sanya
Amesema bado waandishi wa habari wana jukumu la kuchunguza na kutoa taarifa mbalimbali na Serikali itaendelea kusimamia jukumu la kuhakikisha wanafanya kazi kwenye mazingira salama huku akiwataka kufuatilia mabadiliko yaliyopo kwenye sheria mpya ya huduma ya vyombo vya habari.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na walimu kutoka shule kuu ya uandishi wa habari na mawasiliano ya Chuo kikuu cha Dar es salaam (SJMC)

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.