ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, September 18, 2018

GAZETI LA LAHOJI UINGEREZA KUSAIDIA UZAZI WA MPANGO.




CHANZO/MWANANCHI.
Kauli ya Rais John Magufuli kwamba watu wanaodhibiti uzazi ni “wavivu” imezidi kuzua mjadala ambapo gazeti la Daily Mail la Uingereza limehoji kwa nini nchi hiyo iendelea kuipa msaada ambao unahusiana na uzazi wa mpango.
Katika toleo la Jumapili gazeti hilo lilidai kwamba taifa la Afrika ambalo rais wake amesababisha wasiwasi kwa kudai wanawake wanaodhibiti uzazi ni ‘wavivu’ inapewa msaada na Uingereza wa pauni 45 milioni (Sh134.9 bilioni) kwa ajili ya uzazi wa mpango.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya amesema Serikali haijasimamisha kampeni ya uzazi wa mpango kwa sababu kauli ya Rais John Magufuli haijapingana na malengo ya sera ya afya ya uzazi.
Katika majibu yake kwa gazeti dada la The Citizen, Jumamosi Dk Mpoki alisema kwamba katika yote aliyoyasema Rais Magufuli, hakupiga marufuku uzazi wa mpango kama inavyotafsiriwa na baadhi ya watu nchini na wahisani wa kutoka nje.
“Rais aliwataka watu kuzaa idadi ya watoto ambao wanaweza kuwalisha. Maoni yake yalikuwa ni kwamba watu wasilazimishwe kupanga uzazi,” alisema Dk Ulisubisya ikiwa ni siku chache tangu Rais alipotoa kauli hiyo.
Alisema wizara yake na wafadhiri hawaweki masharti ambayo yanazuia idadi ya watoto. Alisema sera ya uzazi wa mpango inalenga kuimarisha afya na ustawi wa mama na mtoto.
Gazeti hilo limesema akiwa katika mkutano wa hadhara wilayani Meatu, Rais Magufuli aliwaambia wananchi kwamba wasikilize ushauri kutoka kwa wageni juu ya uzazi wa mpango kwa sababu wana “nia mbaya”.
Alitoa maoni hayo ya kustaajabisha licha ya ukweli kwamba Idara ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) inamwaga mamilioni ya pauni katika mipango miwili tofauti ili kukuza udhibiti wa uzazi nchini Tanzania.
“Wale wanaofanya mpango wa uzazi ni wavivu. Hawataki kufanya kazi ngumu kulisha familia kubwa na ndiyo sababu wanaamua kudhibiti uzazi na kuishia kuzaa mtoto mmoja au wawili,” alisema.
“Haya ni maoni yangu, lakini sioni haja yoyote ya kutumia dawa za kujizuia kupata watoto. Nimepita Ulaya na mahali pengine nimeona madhara ya kudhibiti uzazi. Katika nchi nyingine sasa wanakabiliwa na tatizo la kupungua idadi ya watu, hawana nguvu ya kutosha.”
Matamshi hayo ya Rais Magufuli yanatarajiwa kukabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka Uingereza iliyoongeza bajeti ya misaada, ambayo ni asilimia 0.7 ya Pato la Taifa - kwa sasa ni pauni 14 bilioni.
Mbunge Peter Bone wa chama cha Conservative kutoka Wellingborough amesema: “Ni vigumu kuamini maoni yake katika siku hizi na umri huu, lakini ikiwa huo ndiyo mtazamo wake kwa nini tunaendelea kupoteza fedha zetu kwa ajili ya kuunga mkono mpango wa uzazi Tanzania?”
Hivi sasa DFID inatenga pauni 153 milioni kwa mwaka kwa miradi nchini Tanzania. Ilizindua mpango unaoitwa Kupanua Upangaji wa Uzazi mwaka jana, ambao una bajeti inayofikia jumla ya pauni 23.5 milioni.
Na mwaka 2014, mpango tofauti na huo uitwa Mpango Mpana wa Uzazi, ulianzishwa kwa bajeti ya jumla ya pauni 22 milioni. Katibu wa Maendeleo ya Kimataifa Penny Mordaunt hata aliwahi kutembelea kitengo cha mpango wa uzazi wakati wa ziara yake ya nchi mwezi uliopita.
Msemaji wa DFID alisema: “Kwa kadri Tanzania inavyokua, ni muhimu kwamba vijana na wanawake wanawezeshwa kufanya udhibiti wa maisha yao, elimu na afya. Mbinu za uzazi wa mpango za Uingereza zinalingana na sera ya taifa ya Tanzania na tunawasiliana mara kwa mara na serikali.”

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.