ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, June 11, 2018

TSNP KUPINGA MAHAKAMANI WANAFUNZI WALIOFUKUZWA BUGANDO.


Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), wameuomba uongozi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya Bugando, kuwarudisha chuoni wanafunzi 10 waliofukuzwa na kusimamishwa chuo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kutaka wanafunzi walipe ada elekezi ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).
Aidha, umedai kuwa kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama Kituo cha sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wataangalia hatua muhimu zaidi, kati ya kukata rufaa chuoni kama ilivyoelekezwa katika sheria za wanafunzi, kupinga uamuzi uliofanyika au kwenda mahakamani.
Wanafunzi hao waliofukuzwa wamo viongozi wa Serikali ya Wanafunzi akiwamo aliyekuwa Rais wa Wanafunzi, Timoth Stephen, aliyekuwa Spika wa Bunge la Wanafunzi 2016/17, Godfrey Lameck na wengine nane waliosimamishwa kwa muda wa miezi tisa.
Wanafunzi hao wanadaiwa kupinga baadhi ya mambo chuoni hapo ikiwamo kuondolewa kwa fedha za faini kwa wanafunzi waliochelewa kulipa ada na kupandisha ada bila kupitishwa na TCU na kukubaliwa na wanafunzi wenyewe.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumapili Juni 10, Mwenyekiti wa TSNP, Abdul Nondo, amesema  kutokana na hali hiyo wanatarajia kuandika barua kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwenda Wizara ya Elimu na TCU kupinga hatua zilizochukuliwa dhidi ya wanafunzi hao.
“Pia tunaomba Wizara ya Elimu na TCU, kuratibu na kutofumbia macho vyuo vya aina hii ambavyo hujiamulia kwa matakwa yao wenyewe, hivyo vyuo vinapaswa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.
“Tunawaomba wadau wote wa elimu, viongozi wakiwamo wabunge, taasisi binafsi na Watanzania kwa ujumla kupinga kwa nguvu zote suala hili na kuomba kwa pamoja ili wanafunzi hao warudishwe chuoni kwani nchi bado inahitaji wasomi wakiwamo madaktari ambao nchi inawasomesha hivyo haiwezekani iwapoteze kwa mtindo wa aina hiyo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.