Video kutoka uwanja wa michezo wa White City unaonesha Bw Mnangagwa akiondoka kwenye jukwaa baada ya kutoa hotuba, mlipuko unapotokea.
Msemaji wake amesema rais huyo alinusurika bila majeraha.
Msemaji wa rais George Charamba ametoa taarifa akisema: "Kumekuwa na majaribio kadha ya kumuua rais miaka mitano iliyopita."
Gazeti la serikali la Herald limeripoti kuwa makamu wa rais Kembo Mohadi ameumia miguuni wakati wa mlipuko huo unaodhaniwa kutokana na bomu, lakini taarifa hizo hazijathibitishwa.
Maafisa wengine wakuu serikali pia wanadaiwa kujeruhiwa, sawa na walinzi wao.
Runinga ya taifa imesema Makamu wa Rais Kembo Mohadi aliumia mguuni.
Ametoa wito kwa raia kudumisha umoja.
Makamu wa Rais wa kwanza wa Zimbabwe Constantino Chiwenga pia alipata majeraha madogo, shirika la habari la Reuters limeripoti.
Mke wake Marry pia ameumia na picha zake akitembelewa na Rais Mnangagwa hospitalini zimesambaa sana mtandaoni.
Gazeti la Herald limetaja mlipuko huo kama jaribio la kumuua rais.
Runinga ya taifa ZBC pia imesema mwenyekiti wa kitaifa wa Zanu PF Oppah Muchinguri-Kashiri, na afisa mkuu wa kisiasa Engelbert Rugeje pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa ZBC walijeruhiwa
Rais Mnangagwa aliingia madarakani Novemba mwaka jana baada ya kuondolewa madarakani kwa Robert Mugabe aliyekuwa ameliongoza taifa hilo kwa miaka 37.
Bw Mnangagwa amekuwa akifanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika 30 Julai ambao utakuwa wa kwanza tangu kuondolewa madarakani kwa Bw Mugabe.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.