ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 23, 2018

PALE SHERIA INAPOWANG'ATA WALIOITUNGA.


CHANZO/MWANANCHI
Katika mgawanyo wa madaraka ya utawala, Bunge ndicho chombo cha kutunga sheria, kuisimamia na kushauri Serikali, Serikali inatekeleza sheria hizo na kusimamia masuala ya utawala na kuleta maendeleo huku mhimili wa tatu wa Mahakama ukipewa jukumu la kutafsiri sheria hizo na kutoa haki.
Bunge likiwa mhimili mmojawapo wa utawala, ni chombo ambacho kimekuwa kikiheshimiwa katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, na hata inapotokea tatizo lolote, wabunge huchukuliwa tofauti na watu wa kada nyingine.
Na mara nyingi, watu mbalimbali kama wabunge, wamekuwa wakiitwa na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kwa tuhuma za kulidharau Bunge.
Bunge likiwa ndio chombo kilichopewa mamlaka ya kutunga sheria, limekuwa likitunga sheria zote zinazotumika nchini na kuridhia nyingine na mikataba ya kimataifa.
Miswada ya sheria iliyo nyingi huwasilishwa na Serikali na mingine na wabunge wenyewe. Miswada hiyo hujadiliwa kwa kina na hatimaye kuipitisha kuwa sheria baada ya marekebisho kadhaa, kama yapo, kisha kusainiwa na Rais na kuanza kutumika.
Sheria ya ‘kupima samaki’
Mwanzoni mwa wiki hii kulitokea sintofahamu ndani ya Bunge wakati watendaji wa Serikali walipokuwa wakitekelezaji moja ya sheria zilizotungwa na chombo hicho, kitendo kilichotafsiriwa kuwa ni kuudharau mhimili huo.
Sakata hilo lilikuwa ni kukamata kwa samaki watatu waliokuwa wamepikwa katika mgahawa wa Bunge, kwa madai kwamba walivuliwa kinyume na sheria.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliagiza maofisa wake kuchunguza samaki wanaouzwa kwenye mgahawa huo. Maofisa hao walienda moja kwa moja kwenye mgahawa na kupima samaki kwa kutumia rula na kubaini samaki watatu waliokuwa hawajafikia kiwango cha kuvuliwa kwa mujibu wa sheria.
Suala hilo lilisambaa kila kona ya Bunge na hata katika mitandao huku kila kitu kikilinganishwa na upimaji kwa kutumia rula hata kama ni chakula.
Ilikuwa ni kama sinema, ingawa mitaani liligeuzwa masihara, maofisa wa Wizara ya Uvuvi walikunja nyuso zao na watu waliokuwapo wakaona jambo hilo si la mzaha.
Katika kuthibitisha kwamba jambo hilo si la utani, kila samaki mmoja aliyekamatwa kwenye mghahawa huo, alisababisha mwendeshaji mgahawa huo kulipa Sh100,000 na hivyo zilimtoka Sh300,000 bila suala hilo kufika mahakamani.
Waliotunga sheria wakerwa
Kitendo cha kuvamia mgahawa wa Bunge na kupima kitoweo, kiliwakera wabunge na kufikisha suala hilo ndani ya chombo hicho.
Ingawa suala la maofisa wa uvuvi kuwanyanyasa wavuvi na watu wengine wanaokamatwa na samaki limezungumzwa mara nyingi bungeni, safari hii lilipata mguso wa pekee na kutisha jamii.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba ndiye alikuwa wa kwanza kuhamisha mada hiyo kutoka mgahawani kwenda ndani ya ukumbi wa Bunge ambako wabunge ‘waliishambulia’ na kusababisha kiti cha Spika kuagiza Serikali itoe taarifa, tukio ambalo liliisha kwa Waziri Mpina kuomba radhi.
Mpina aomba radhi
Ilichukua siku moja kwa Mpina kuomba radhi baada ya kelele za wabunge kuongezeka na mizaha kujaa kwenye mitandao ya kijamii. Alikiri kuwa alikuwa ametumia vibaya sheria husika katika ukamataji wa samaki hao katika eneo ambalo lilipaswa kuombewa kibali kwanza.
Katika tamko lake, Mpima anasema watumishi wa wizara yake waliingia bila ya kibali maalumu na kumhoji mmiliki wa mgahawa huo na kuwapima samaki hao ambao walibaini kuwa walikuwa chini ya sentimeta 25 zinazotakiwa.
“Napenda kukiri kuwa, watumishi katika kutimiza wajibu wao, waliingia bila kibali, kupima chakula kilichopikwa na kwa taratibu hizo. Wizara inaliomba radhi Bunge lako tukufu na wewe Mheshimiwa Spika, na wizara haikuwa na nia mbaya katika jambo hilo,” alisema Mpina.
Pamoja na Spika Job Ndugai kutoa msamaha huo, alizungumza kwa njia ambayo ilionyesha kuwa jambo hilo halikuwa limefurahisha zaidi.
Ndugai alisema katika jambo hilo alikuwa amekasirishwa zaidi kwa kuwa lilikuwa limelidhalilisha Bunge na kwamba mabunge ya nchi nyingine yakisikia kuwa kuna jambo kama hilo limetokea Tanzania yatashangaa kwa kuwa yalipaswa kujifunza hapa.
Mpina akosa mtetezi
Kila mbunge aliyesimama kuzungumzia suala hilo alionyesha kukerwa na kitendo kilichofanywa na Mpina ambaye hata katika mjadala wa bajeti yake, wengine walienda mbali wakisema amejaa kiburi na majivuno.
Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku (Msukuma) ambaye amewahi kueleza kuwa ni mwathirika wa operesheni ya kupambana na uvuvi haramu, alieleza kuwa Mpina ameshindwa kabisa kutumia elimu yake ya uchumi na akashauri kuwa iko haja ya kuangalia vyeti vyake.
Msukuma alikwenda mbali akieleza kuwa mambo hayo kufanyika kwake yanatokana na mbio za urais anazozitaka waziri huyo ambaye aliomba uteuzi wa CCM mwaka 2015.
Lakini, mbunge huyo alihitimisha kuwa Mpina hataweza kuipata nafasi hiyo ya juu katika nchi.
Sheria yawang’ata walioitunga
Pamoja na hoja zote ndani na nje ya Bunge, wabunge wengi wanaizungumzia sheria waliyotunga wao katika mitazamo tofauti, baadhi wakisema haina shida huku wengine wakisema ni mbovu.
Mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga alisema sheria ya kupambana na uvuvi haramu ni mbovu na ilishapingwa na wabunge tangu muda mrefu, lakini kuna baadhi yao walilazimisha ipitishwe.
Kalanga anasema ugumu wa utekelezaji wa sheria hiyo waliuona mapema, lakini wengine hawakauona hadi walipotendewa kile walichoona kinawagusa wao.
Anasema kama ni udhalilishaji, wananchi walishalizwa kwa muda mrefu.
“Tuliipinga sheria hii kwa nguvu zote, ikapitishwa, leo hii imeligusa Bunge wameanza kulalamika. Lakini hawajui kuwa wananchi walishalizwa kwa muda mrefu na bado wanaendelea kulizwa,” alisema Kalanga.
“Naona hakuna haja kuibadili kwa pupa, badala yake tujifunze kuziangalia sheria zote kabla ya kupitishwa.”
Lakini, mbunge wa Mafia (CCM), Mbaraka Dau anamtaka Waziri Mpina kutambua kwamba kuna samaki ambao kimazingira hawawezi kufikia sentimita 25, hivyo kitendo cha kukamata kila samaki bila ya kujua wapi walikotoka hakitasaidia bali kuumiza wananchi.
Dau anasema sekta ya uvuvi ilishasaulika na hata katika bajeti imetengewa asilimia 0.01 ya fedha za maendeleo na kwamba kuna tatizo kubwa katika eneo hilo.
“Mimi ningeomba kule Mafia kuna kiwanda kikubwa cha kuchakata samaki, walikuwa wanafanyia kazi tani 20 hadi tani 30 kwa mwezi, lakini kwa matamko ya sasa yaliyokuja wanataka kukifunga,” alisema Dau.
“Kuna samaki hawezi kufikia sentimita 25, Waziri njooni mje muongee na wavuvi muwaeleze, kila samaki wakipelekwa wanakuwa ‘reject’ (hawafiki ukubwa), njooni kwani samaki wengine hawafikii sentimita hizo.”
Mbunge wa Babati Vijiji (CCM), Jitu Son alisema sheria ni nzuri lakini utekelezaji wake umekuwa ni kero na kumtaka Waziri Mpina kutafakari na kuangalia namna anavyoweza kutumia mamlaka yake katika kutekeleza sheria za Bunge bila kuwakera watu
Mbunge huyo alisema katika hali ya kawaida haiwezekani Waziri kuingia kwenye migahawa na kuanza kupima samaki waliopikwa wakati sheria inasema apambane na uvuvi haramu siyo upishi haramu.
Anataka jambo hilo liangaliwe kwa mapana na wizara itengewe fungu la kutosha kwa ajili ya kutoa elimu kwa Watanzania wote, vinginevyo wataumiza zaidi watu wa hali ya chini.
Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea alisema sheria hiyo ina mapungufu makubwa na inapaswa kubadilishwa haraka kwa kuwa hata kanuni zikitungwa kwa hekima, bado kutakuwa na shida katika utekelezaji wake.
Mtolea alimshukia waziri kuwa angeweza kuifanya sheria iwe na unafuu kwani haisemi kuwa ashughulike na samaki wa jikoni badala yake anapaswa kushughulika na wavuvi haramu, hivyo angeweza kujipambanua katika utekelezaji lakini anatekeleza kwa kufuata mihemuko.
“Kuna samaki wengine hawakui na wengine ni wa kufugwa kwenye mabwawa, hivyo hawezi kulazimisha mfugaji atunze samaki wake hadi wafikie ukubwa wanaoutaka wao wakati si mali yao. Je, katika maeneo ambayo samaki hawakui nako hali ni hivyohivyo?” alihoji Mtolea.
Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatale, huku akimtaka Waziri Mpina ajitathmini, alisema sheria hiyo inalazimisha hata wavuvi wadogo kutembea na rula kupima kila samaki wanaomnasa.
Lwakatale anasema kama jambo hilo halitaangaliwa kwa mpana na kusimamiwa ipaswavyo, linaweza kupeleka kilio kikubwa kwa Watanzania wa hali ya chini na masikini wasiokuwa na hatia, hasa ambao uvuvi ni sehemu ya maisha yao.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, hakuna namna yoyote ambayo Bunge linaweza kujitetea katika maisha ya Watanzania kwa kuwa mfano ulioonyeshwa na Mpina ni maumivu na kilio kwa watu wa chini kama wafugaji na wajasiriamali.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.