ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, May 31, 2018

ZIDANE AACHIA NGAZI REAL MADRID, WENGER ATAJWA KUMRITHI.

KOCHA Mfaransa, Zinedine Zidane amejiuzulu ukocha wa Real Madrid baada ya kuiongoza timu kutwaa mataji matatu ya kihistoria ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mchezaji huyo wa zamani wa klabu hiyo, aliitisha mkutano na Waandishi wa Habari leo ghafla akisema kwamba ataondoka baada ya miaka miwili na nusu kazini.

Zidane mwenye umri wa miaka 45 na gwiji wa klabu kama mchezaji na kocha amesema anafikiri huu ni wakati mwafaka kuondoka.

Makocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger, kocha wa sasa wa Chelsea, Antonio Conte na wa Tottenham, Mauricio Pochettino wapo mstari wa mbele katika kuwania nafasi hiyo.

Akiwa ameongozana na Rais wa Real, Florentino Perez, Zidane alisema: "Nimechukua uamuzi wa kutoendelea msimu ujao. Kwangu mimi na kwa mtu yeyote, nafikiri wakati wa mabadiliko umefika. Haukuwa uamuzi mwepesi,".

Zidane alimuambia Perez mpango wake huo Jumatano. "Naipenda hii klabu, nampenda rais,"amesema. "Alinipa nafasi ya kuja kama mchezaji na sasa kocha na ninajivunia. Lakini tunatakiwa kubadilika.

"Nitakuwa karibu na hii klabu kwa maisha yangu yote yaliyobaki. Ninataka kuwashukuru mashabiki, ambao wakati wote wamenisapoti nikiwa kama mchezaji na kocha. Kulikuwa kuna wakati mgumu katika msimu na pia kuna wakati nilikubaliana na hali halisi, ninataka kuwashukuru mashabiki,".

Zidane, kiungo wa zamani wa Real, Juventus na Bordeaux inafahamika alikuwa ana mkataba Madrid hadi mwaka 2020.

Baada ya kujiuzulu ukocha wa kikosi cha vijana cha Real Madrid, kijulikanacho kama Castilla B, akaenda kuchukua nafasi ya Rafa Benitez kikosi cha kwanza Januari mwaka 2016 na mwishoni mwa msimu Real ikamaliza nafasi ya pili nyuma ya Barcelona katika La Liga.

Akatwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa penalti 5–3 baada ya sare ya 1–1 mjini Milan.

Zidane akaongeza taji la La Liga Juni 2017 kabla ya kutetea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuifunga 4-1 Juventus mjini Cardiff. 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.