Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jaffo, akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Dodoma, akielekeza Mikoa kukusanya takwimu sahihi za Wazee (Picha na Atley Kuni- OR TAMISEMI)
Serikali yaandaa utaratibu wa Kuwatambua Wazee nchini
Na. Atley Kuni na
Mathew Kwembe, OR TAMISEMI
Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo
amewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia zoezi la kuwatambua wazee wote nchini
katika mikoa yao na wahakikishe kuwa ifikapo tarehe 30 Juni, 2018 Mikoa yao
inawasilisha Ofisi ya Rais TAMISEMI orodha ya wazee katika mikoa yao.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma leo, Mhe. Jafo alisema kuwa tayari amekwishatoa maagizo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha kuwa zoezi hilo linashirikisha ngazi zote za Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Alisema ifikapo tarehe 15 juni 2018 anatarajia kuona kuwa zoezi hilo liwe limekamilika katika ngazi ya kata ambapo Mtendaji wa Kata atapaswa kuliwasilisha katika ngazi ya halmashauri kabla ya kufika ngazi ya Mkoa.
Pia alisema kuwa ifikapo tarehe 20 Juni, 2018 anatarajia kuwa zoezi hilo liwe limekamilika katika ngazi ya halmashauri ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri atapaswa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji katika ngazi ya mkoa tarehe 26 juni, 2018.
Waziri Jafo alieleza kuwa ifikapo tarehe 30 Juni, 2018 anatarajia kuwa ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa iwasilishe taarifa hiyo katika Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Akifafanua zaidi kuhusu umuhimu wa zoezi hilo Mhe.Jafo alisema kuwa serikali imeamua kuchukua hatua hiyo ya kuwatambua wazee wote nchini ili wasiendelee kupata manyanyaso kwa kukosa utambuzi rasmi.
Aliongeza kuwa wazee ni tunu ya taifa na hivyo hawana budi kuenziwa kwa serikali kuhakikisha kuwa wanatambuliwa na kupatiwa vitambulisho vitakavyowawezesha kupata huduma muhimu kama vile afya.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo wazee wanaolengwa ni wale wa kuanzia miaka 60 ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 75 ya wazee wote nchini wapo maeneo ya vijijini.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.