ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, March 20, 2018

MUUNGANO WA MAKANISA KENYA: ASILIMIA KUBWA YA WAKRISTO NI WACHAWI NA WASHIRIKINA.

Muungano wa makanisa nchini Kenya umetangaza kuwa, uchawi na ushirikina umekumbatiwa zaidi na Wakenya, kuliko wanavyomuamini Mungu.
Hayo yamesemwa na Askofu Peter Mburu, mwenyekiti wa muungano huo katika kongamano lililopewa jina la kuombea taifa katika uwanja wa Safaricom Kasarani jijini Nairobi na kuongeza kuwa, uchawi na ushirikina kwa ajili ya kusaka maisha mazuri, utajiri na vyeo, ni mambo ambayo yamekumbatiwa sana na Wakristo. Kwa mujibu wa Askofu Mburu, asilimia kubwa ya wafanyabiashara, wafanyakazi katika nyadhifa tofauti za umma na binafsi, wanasiasa na wengine wengi wameshikamana na uchawi kwa kuutumia kama kinga yao ya maisha.
Wafuasi wa dini ya Kikristo wakiwa kanisani
“Katika muungano wetu tumeweza kuwasimamisha kazi jumla ya wahubiri 23 tangu Januari 2017 baada ya kunaswa wakishiriki vitendo vya ushirikina. Waumini wetu wengi wamekiri waziwazi kwamba, wanajihusisha na ushirikina ili kujipa ahueni ya kimaisha,” Amasema Askofu Mburu. Kongamano hilo ambalo linamalizika leo Jumanne limetuma ujumbe kwa ofisi za serikali, mabunge na asasi nyingine kwamba ndani ya idara hizo kunashuhudiwa kiwango kikubwa cha uchawi na ushirikina. Kwa upande wake Padri Joseph Wamalwa wa Kanisa Katoliki Kaunti ya Nairobi amesema kuwa ongezeko la ushirikina na uchawi miongoni mwa Wakenya linadhihirika kutokana na visa mbalimbali vinavyoshuhudiwa kila mara ikiwemo vitendo vya kulishwa nyasi, matukio ya unyofoaji kiholela wa sehemu za siri na pia mauaji ya walemavu wa ngozi (Zeruzeru), huku Wakristo wengi wakinaswa wakiwa wamevaa hirizi mwilini kwa dhana ya kujikinga na mikosi ya kijamii, kiuchumi au kisiasa.
Sehemu ya uchawi 
Padri Wamalwa amefafanua zaidi kwa kusema, mwaka jana  Shirika la The Pew Research Centre la nchini Marekani lilitoa ripoti ikionyesha kuwa, Wakenya wengi bado wanaabudu miungu ya jadi, kutoa kafara, kujihusisha na ushirikina mbalimbali sambamba na kuamini mapepo ya kuzimu. Amesema: “Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Kenya iko mbele kuliko nchi kama Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Ethiopia, Nigeria, Zambia na Rwanda katika kuamini ushirikina na uchawi.” Pia amesema, asilimia kubwa ya Wakristo na Wakenya waliohojiwa wamekiri kuvaa hirizi na pia kwenda kwa waganga wa kienyeji.
CHANZO:-http://parstoday.com/sw/news/africa

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.