ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, March 28, 2018

JICHO LA SERIKALI KATIKA USIMAMIZI WA FEDHA NCHINI TANZANIA

FMOs Wakumbushwa Utendaji wao
Na. Atley Kuni, OR TAMISEMI
Maafisa Usimamizi wa Fedha (Finance Management Officers - FMOs) kutoka Sekretarieti za Mikoa yote ya Tanzania Bara wamesisitizwa kuwa jicho la usimamizi wa fedha za Halmashauri na kutoa taarifa kwa Katibu Tawala (RAS) pamoja na ngazi ya Wizara ili kuwa na taarifa sahihi za kifedha kuanzia ngazi ya Halmashauri, Mkoa na Wizara.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Charles E. Mhina wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji wa Fedha zinazopelekwa Mamlaka za Serikali za Mitaa (Fiscal Transfer Tracking Monitoring(FTTM) – Web Portal)  yanayowakutanisha FMOs kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara kuanzia tarehe 27-28 Machi, 2018 kwenye ukumbi wa Maabara ya Kompyuta uliopo katika jengo la Sokoine OR TAMISEMI, mjini Dodoma.

Dkt. Mhina amewahimiza Wataalam hao kuwa eneo la utoaji wa taarifa ni muhimu sana ili kuwa na taarifa sahihi zitakazosaidia kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.

“Tulichobaini kama Wizara kuna umuhimu wa kuimarisha daraja la mawasiliano kati ya FMOs na Halmashauri. FMOs mmekuwa mkitoa taarifa kwa RAS na Wizara, huku mkisahau kwamba nyinyi kama wataalam mnatakiwa kuzisimamia na kuzijengea uwezo Halmashauri pia.” amesema Dkt. Mhina na kuongeza kuwa changamoto zilizopo zianishwe na kutumika kama chachu yakuleta mabadiliko.

“Changamoto ya matumizi sahihi ya mfumo wa FTTM – Web Portal kutokana na ukosefu wa mafunzo imekuwepo toka 2015. Sasa tumieni fursa hii ya mafunzo mtakayoyapata kikamilifu ilimtakapo ondoka hapa mlete mabadiliko chanya katika usimamizi wa fedha. Wataalam wetu wa TEHAMA na FEDHA kutoka OR TAMISEMI wapo tayari na wamejipanga kuwaelekeza kikamilifu.” alisema Dkt. Mhina.

Pamoja Wataalam hao kusisitizwa juu ya mfumo wa FTTM-Web Portal, Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA OR TAMISEMI, Ndg. Erick Kitali  hakusita pia kuwakumbusha Wataalam hao kuwa ifikapo Julai Mosi, 2018 Mamlaka zote za Serikali za Mitaa zitumie  toleo jipya la 10 la Mfumo wa Malipo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa  (Epicor 10) ili kwenda sambamba na mahitaji ya sasa.

Ndg. Kitali amewaambia wataalam hao kuwa OR TAMISEMI katika utendaji wake wa kazi hutegemea sana ushauri wa Wataalam kutoka ngazi za msingi ambapo ndipo walipo wananchi. Hivyo, aliwataka Wataalam hao kuzingatia mafunzo yatakayotolewa ili kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Maafisa Usimamizi wa Fedha (Finance Management Officers - FMOs) kutoka Sekretarieti za Mikoa hutumika kama wataalam washauri katika ngazi ya Mkoa ili kuzisaidia Halamashauri juu ya taarifa mbali mbali za kifedha sambamba na kumshauri katika katibu Tawala pamoja na Wizara juu ya mwenendo wa kifedha katika mkoa husika.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.