ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, February 3, 2018

YANGA YAILIPUA LIPULI NYUMBANI KWAO 2-0.


YANGA SC imejivuta kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Lipuli Uwanja wa Samora mjini Iringa.

Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 31 baada ya kucheza mechi 16, ikipanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, sasa ikiwazidi kwa pointi Azam FC ambao wanacheza mechi yao ya 16 usiku dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Yanga pia imepunguza pengo la pointi inazozidiwa na vinara, Simba SC hadi kubaki tano – lakini Wekundu wa Msimbazi nao watacheza mechi yao ya 16 kesho dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Erick Onoka aliyesaidiwa na Geoffrey Kihwilio na Janeth Balama, Yanga ilipata bao moja kila kipindi.

Na mabao hayo yalikuja baada ya Yanga kupata pigo dakika ya 17 kufuatia kipa wake wa kwanza Mcameroon, Youthe Rostand kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na chipukizi, Ramadhan Awam Kabwili.

Kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Papy Kabamba Tshishimbi alifunga bao la kwanza dakika ya 19 kwa kichwa akimalizia mpira uliotemwa na kipa Agathon Anthony Mkwando baada ya kichwa cha kuparaza cha winga Emmanuel Martin kufuatia kona ya kiungo Pius Charles Buswita

Kipindi cha pili, Yanga ya kocha Mzambia, George Lwandamina ilirudi na mchezo mzuri na kufanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na Buswita dakika ya 55, aliyempiga chenga kipa Mkwando baada ya pasi nzuri mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa kutokea pembeni kulia na kufunga bao zuri.

Yanga ilijitahidi kuendelea kusaka mabao zaidi, lakini Lipuli walikuwa imara na kumaliza mchezo kwa kipigo cha mabao 2-0.

Lipuli FC; Agathon Mkwando, Stephen Mganga, Ally Mtoni, Martin Kazila, Joseph Owino, Novaty Lufunga, Seif Karihe/Tola Mangonela dk69, Mussa Nampaka/Zawadi Mawiya dk71, Adam Salamba, Malimi Busungu na Jamal Mnyate/Jerome Lembele dk78.

Yanga SC; Youthe Rostand/Ramadhani Kabwili dk17, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, Papy Kabamba Tshishimbi, Emmanuel Martin, Raphael Daudi/Raphael Daudi dk86, Obrey Chirwa, Pius Buswita na Geoffrey Mwashiuya/Maka Edward dk81.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.