ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, January 22, 2018

MKURUGENZI WA NGO YA MWANZA NA WENZAKE 9 WANASWA NA TAKUKURU KWA UTAPELI.

Mkuu wa TAKUKURU mkoani Mwanza, Ernest Makale akizungumza na wanahabari hii leo.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Mwanza, imemtia nguvuni Andrea Mabagala (70) ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali liitwalo Popular Culture Youth and Sports Organization PCYSO na wenzake tisa kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na kuomba na kupokea rushwa kinyume cha sheria.
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mwanza, Ernest Makale amewataja watuhumiwa wengine kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji George Mashimba, Afisa Utumishi Mkuu Fred Tingatinga, Mkuu wa Idara ya Kanda Felix Lugakingila, Mhasibu Mkuu Lilian Lwelamila, Mhasibu Abdallah Waziri, Meneja Miradi Edga Shinyanga, Mkaguzi wa Kanda Antony Msemakweli pamoja na Waratibu Watendaji wa Kanda ambao ni Mary Maswe na Asha Mzinga.
Mkuu wa TAKUKURU mkoani Mwanza, Ernest Makale akizungumza na wanahabari hii leo.
Mtuhumiwa mwingine aliyetiwa nguvuni ni Robert Kasili (65) ambaye amewahi kukamatwa na Takukuru julai 2017 kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na kupokea rushwa ya shilingi 70,000 kutoka kwa mwananchi mmoja kwa ahadi ya kumpatia ajira ambapo shitaka hilo lilifikishwa mahakamani na mtuhumiwa kuachiwa kwa dhamana.
Amesema watuhumiwa hao walikamatwa na maafisa wa Takukuru ijumaa iliyopita Januari 19 katika ofisi za shirika hilo zilizopo Nyakato Mecco Jijini Mwanza ambapo watuhumiwa hao kupitia shirika hilo wanadai kufanya shughuli za kuwasaidia watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, akina mama pamoja na watoto.
Makale amebainisha kwamba kati ya mwaka 2014 hadi julai 2017 watuhumiwa hao wamejipatia zaidi ya shilingi Milioni 24 kutoka kwa wananchi 800 ambao waliwasajili kwa kuwatoza fedha kila mmoja shilingi elfu 30,000 kama gharama za maombi ya kazi hewa iliyotangazwa na shirika hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la PCYSO akifafanua jambo kwa wanahabari baada ya yeye na wenzake kutiwa nguvuni na TAKUKURU mkoani Mwanza.
Ameongeza kwamba mbali na 30,000 zilizotolewa kama ada ya maombi, wananchi hao kila mmoja kwa nyakati tofauti, walitoa rushwa kwa kiwango cha kati ya shilingi 300,0000 hadi 1,000,0000 kwa viongozi wa shirika hilo ili kupata kazi na wengine kuendelea kulinda ajira walizoahidiwa.
Inaelezwa kwamba shirika hilo kila mwezi limekuwa likifanya malipo hewa ya mishahara kwa wafanyakazi wake yenye jumla ya shilingi bilioni moja huku fedha hizo zikisubiliwa kulipwa pindi mfadhili waliyemtaja kuwa ni Shirika la Afya Duniani WHO atakapotoa pesa jambo linalofanya shirika hilo kuwa na madeni yanayokadiliwa kufikia bilioni 60.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la PCYSO akifafanua jambo kwa wanahabari baada ya yeye na wenzake kutiwa nguvuni na TAKUKURU mkoani Mwanza.
Watuhumiwa wote 10 wako rumande na watafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika ambapo Takukuru inawatahadharisha wananchi kuwa makini na matapeli na kwamba wafahamu kutoa na kupokea rushwa ni kosa la jinai hivyo kila mmoja awajibike kukemea vitendo hivyo.


Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.