ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, December 16, 2017

WALIOACHIA MAENEO KUPISHA MGODI WATAKIWA KULIPWA FIDIA

 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mang'onyi, Kata ya Mang'onyi, wilayani Ikungi waliosimamisha msafara wake (hawapo pichani)

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mang'onyi, Kata ya Mang'onyi, wilayani Ikungi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani).

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (mbele katikati) akiwa nyumbani kwa Mzee Bastan Mtundwi (mbele kulia) na mkewe Esta Mtundwi ambao walijengewa Nyumba na Kampuni ya Shanta ikiwa ni fidia ya kupisha eneo.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mang'onyi, Kata ya Mang'onyi, wilayani Ikungi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani).

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akimsikiliza  Meneja wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Shanta Mining Limited, Mhandisi Philbert Rweyamamu (aliyesimama) akielezea shughuli na mkakati wa kampuni yake.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na Wafanyakazi wa Kampuni ya Shanta Mining Limited (hawapo pichani) alipotembelea eneo linalomilikiwa na kampuni hiyo.

SHANTA MINING YATAKIWA KUKAMILISHA ULIPAJI FIDIA

Serikali imeiagiza Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Shanta Mining Limited inayofanya shughuli zake Mkoani Singida kuharakisha ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha maeneo yao ili shughuli za uchimbaji zianze mara moja.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alitoa agizo hilo Desemba 12, 2017 wakati wa ziara yake ya kutembelea migodi ya dhahabu katika wilaya za Ikungi na Manyoni ili kujionea shughuli zinazoendelea pamoja na kuzungumza na wachimbaji wa madini.

“Mchakato wa fidia ufanyike haraka na mgodi uanze shughuli zake za uchimbaji mapema,” aliagiza Naibu Waziri Nyongo.

Akiwa njiani kuelekea kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Elizabeth Shango uliopo katika Kijiji cha Sambaru, msafara wake ulisimamishwa na wananchi katika Kijiji cha Mang'onyi, Kata ya Mang'onyi, wilayani Ikungi ambao walilalamika kuzuiwa kuendeleza maeneo yao na kampuni hiyo na huku wakicheleweshewa kulipwa fidia.

Walisema kuwa tayari wameachia maeneo waliyokuwa wakimiliki kwa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo kilimo na uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu ili kupisha shughuli za uchimbaji mkubwa lakini Kampuni hiyo ya Shanta bado haijakamilisha ulipaji wa fidia.

Wananchi hao vilevile walimuomba Naibu Waziri Nyongo kuiagiza kampuni hiyo kuwapatia maeneo yaliyo wazi ili wafanye shughuli za uchimbaji.

Kufuatia malalamiko hayo, Naibu Waziri Nyongo aliiagiza kampuni hiyo kuhakikisha inakamilisha taratibu za ulipaji wa fidia bila kuchelewa ili shughuli za uchimbaji zianze mapema iwezekanavyo.

“Wananchi wanayo hoja ya msingi na inapasa wasikilizwe, ili taratibu zifanyike bila kuwepo migongano isiyokuwa ya lazima,” alisema.

Aliiagiza kampuni hiyo kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo pamoja na Uongozi wa Vijiji  kujenga mahusiano bora baina yao na wananchi.

Nyongo alisema ili kupunguza migogoro baina ya kampuni na wananchi ni busara wakapatiwa maeneo ili wafanye shughuli za uchimbaji.

“Wapeni na wao maeneo wachimbe, busara itumike kuwapatia maeneo mazuri ili kujenga mahusiano mazuri,” aliagiza Naibu Waziri Nyongo.

Kwa upande wake Meneja wa Kampuni hiyo, Mhandisi Philbert Rweyamamu alisema kuchelewa kwa mchakato wa ulipaji fidia kumetokana na migongano ya kijamii.

Alisema kutokana na wananchi kutokuwa na elimu sahihi ya faida ya mradi wamekuwa wakileta vikwazo katika hatua mbalimbali za mchakato wa fidia.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.