Naibu Waziri Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akizungumza na wataalamu wa
ardhi, viongozi na watendaji wa halmashauri ya Wilaya na Manispaa ya Singida
[hawapo pichani], Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi.
Naibu Waziri Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akizungumza na wananchi wa
kijiji cha Singa tarafa ya Kinampundu Wilayani Mkalama, Kulia kwake ni Mkuu wa
Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jaksoni Massaka.
Naibu Waziri Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akisikiliza maelezo kutoka
kwa Afisa Ardhi wa Wilaya ya Iramba Lugano Sanga kuhusu utuzanji wa nyaraka za
idara hiyo.
SERIKALI kupitia
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeahidi kutoa timu ya wataalamu
watakao suluhisha mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida na Wilaya
ya Hanang’ Mkoani Manyara.
Naibu Waziri Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula ametoa ahadi hiyo wakati wa
ziara yake Mkoani Singida katika kijiji cha Singa tarafa ya Kinampundu Wilayani
Mkalama ambapo amesema Wizara yake itatoa wataalamu watakaoweza kutatua mgogoro
huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 30.
“Kwakuwa pande zote
mbili za Mkalama na Hanang’ zimekutana mara kadhaa bila mafanikio, nitaleta
wataalamu wafike eneo la mpaka ili wataalam hao wawasomee alama moja baada ya
nyingine, kila mmoja wenu afahamu eneo lake mwisho ni wapi, nadhani hapo
tutakuwa tumewasaidia wananchi wetu”, amesema Dkt Mabula.
Amesema wananchi wa
Kijiji hicho cha Singa wasiwe na wasiwasi endapo baada ya kuonyesha mpaka wao
mashamba yao yakionekana yapo wilaya ya Hanang’ wataruhusiwa kuendelea
kuyamiliki ila watatakiwa kwenda kujitambulisha katika Uongozi wa Wilaya hiyo.
Aidha Dkt Mabula
amesema timu hiyo ya wataalamu itahakikisha inasuluhisha migogoro yote ya
mipaka ya wilaya hiyo ambayo ngazi ya wilaya imeshindikana kutatuliwa.
Amewashauri wananchi
hao kutouza au kugawa ardhi yao ovyo ovyo kwakuwa ardhi ni mali na mtaji popote
pale hata kama ni vijijini hivyo watunze ardhi yao na kuiongezea thamani kwa
kuipima na kuwa na hati ya umiliki.
Baadhi ya wananchi wa
kijiji hicho walitoa malalamiko kwa Naibu Waziri huyo huku wakimueleza kuwa
mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu umesababisha baadhi yao kupelekwa
mahakamani kwa madai ya kuvamia mashamba.
Mzee Anaftali Amosi
Majii amemueleza Naibu waziri kuwa taarifa za mgogoro huo zilitolewa muda mrefu
na kuongeza kuwa wananchi wamechoka kushitakiwa kwa makosa ya uvamizi wa
mashamba wakati wao wanaamini wanayamiliki kwa uhalali jambo ambalo
linawachelewesha kimaendeleo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama Mhandisi Geofrey Sanga amesema Wilaya ya
Mkalama ina migogoro ya mipaka kwa wilaya tano zinazowazunguka.
Mhandisi Sanga
ameeleza kuwa Mkalama ina migogoro ya mipaka kati yake na Wilaya za Mbulu,
Iramba, Hanang’ na Wilaya ya Singida jambo ambalo linawafanya baadhi ya
wananchi kukwepa kuchangia shughuli za maendeleo wakidai wao sio wa Wilaya
hiyo.
Wakati huo huo Naibu
Waziri Dkt Angelina Mabula amefanya ziara Wilaya ya Iramba na kufanya ukaguzi
wa kushtukiza katika masijala ya Ardhi ya Wilaya hiyo ambapo hakuridhishwa na
utunzaji wa nyaraka pamoja na utendaji usioridhisha unaosababisha wananchi
kuchelewa kupata hati za viwanja.
Dkt Mabula pia
hakuridhishwa na kasi ndogo ya upimaji viwanja na utoaji wa hati wilayani humo
huku akiwataka kuacha kukusanya kodi mbalimbali za ardhi kwa utendaji wa
kimazoea bali wafanye kazi bidii.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.