Mkuu wa Wilaya ya
Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akisisitiza jambo wakati wa kikao Cha kazi na
wataalamu wa Kilimo, Mifugo, Ardhi, Maliasili na mazingira.
Wataalamu wa kilimo,
Mifugo, Ardhi, Maliasili na mazingira wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Wilaya
ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wakati wa kikao cha kazi.
Afisa Kilimo na
Mifugo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ayoub Sengo (aliyesimama) akizungumza
jambo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu, Mwingine ni
Afisa Tawala Wilaya ya Ikungi Dandala Mzunguor.
Wataalamu wa kilimo,
Mifugo, Ardhi, Maliasili na mazingira wakishauri jambo wakati wa kikao kazi na
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu.
Na
Mathias Canal, Singida
Mkuu wa Wilaya ya
Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu amekutana na kufanya kikao cha kazi na wataalamu
wa Kilimo, Mifugo, Ardhi, Maliasili na mazingira kubaini kwa pamoja mbinu bora
za kuwasaidia wakulima kuzalisha mazao ya chakula na biashara kwa wingi.
Katika kikao hicho
kilichohudhuriwa na Maafisa kilimo na Mifugo, Maafisa Ardhi, Maliasili na
Mazingira, Maafisa Ugavi wa Kata sambamba na Maafisa Tarafa, Mtaturu amesema
kuwa bado uzalishaji wa mazao ni mdogo katika Wilaya ya Ikungi ukilinganisha na
hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kuwa na ardhi nzuri.
Amewataka wataalamu
hao wa kilimo kuwasaidia wakulima ili kuiwezesha Sekta ya Kilimo, kutoka kilimo
cha kujikimu kuwa kilimo cha kibiashara, kitakachowezesha kukuza uchumi wa mtu
mmoja mmoja na kupunguza umasikini kwa watanzania Sambamba na kujitosheleza kwa
chakula.
Mtaturu amesema ili kilimo
kiwe kizuri na chenye tija kwa wananchi, Wataalamu wanapaswa kuzingatia uwepo
wa pembejeo na mbegu bora za kisasa na kuhuisha kilimo cha umwagiliaji kwa
kuandaa mpango wa kujenga skimu za umwagiliaji.
Ameongeza kuwa serikali
imetoa tani 20 za mbegu za kamba katika Wilaya ya Ikungi ili kuongeza
uzalishaji wa zao hilo ambapo zitagawanywa kwa wakulima ili msimu wa kilimo
unapoanza tayari kusiwe na kucheleweshwa kwa mbegu hizo.
Pia amewaagiza
maafisa ugani kuwa na mashamba darasa kwani kupitia wao yatawasaidia wakulima
kuwa na uelewa mkubwa katika kuongeza ufanisi wa kilimo chenye tija.
Aidha, amesema Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imeanzisha huduma zake kanda ya Kati Dodoma ambapo
mikopo ya aina mbalimbali hutolewa kuwezesha wakulima kuongeza tija na
uzalishaji katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Mtaturu amesema ni
vyema kama wataalamu wa kilimo watatumia nafasi hiyo kuwaunganisha wakulima na
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kusaidia upatikanaji
wa Masoko na kuongeza Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo.
Katika kikao hicho cha
kuwakumbusha majukumu wataalamu hao Mtaturu amewataka kuandaa mpango kazi wa
mazao ya kilimo hususani mazao ya chakula na biashara.
Mtaturu amewaelekeza
wataalamu hao wa kilimo kuwasisitiza wananchi katika maeneo yao kuanza kulima
mazao ya kipaumbele yaliyoelekezwa na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa ambayo ni
zao la Pamba, Korosho, Chai, Kahawa na Tumbaku.
Amesema pomoja na
mazao hayo ya kipaumbele lakini pia wananchi wanapaswa kuendelea kuongeza nguvu
katika mazao yanayostawi kwa wingi Wilayani humo ikiwa ni pamoja na zao la
alizeti, mtama, mahindi na zao la dengu.
Katika upande
mwingine Mtaturu ameshauri wataalamu wa Mifugo kutilia msisitizo Ufugaji wa
kisasa (Ziro Grazing) kwa kutembelea na kupata utaalamu wa Ufugaji na mbegu
Bora za ya Ng'ombe wa kisasa kwa wataalamu katika Rachi ya Taifa ya Kongwa
(NARCO) na LITI iliyopo Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Sambamba na hayo pia
Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza heka 1500 ambazo ni kichaka kuandaliwa utaratibu
kwa ajili ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa kilimo.
Naye Afisa Kilimo na
Mifugo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ndg Ayoub Sengo amepongeza kasi ya
uwajibikaji ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu kwa ufanisi wake
kusaidia kuonyesha njia jambo ambalo linapelekea kubadili fikra za wakulima na
wananchi kwa ujumla.
Sengo amempongeza
Mkuu huyo wa Wilaya ya Ikungi kwa kuwezesha kupatikana muwekezaji ambaye atakayepewa
heka 1000 na serikali ya kijiji kwa ajili ya kilimo cha korosho zao ambalo
litakuwa na tija kwa pande zote mbili kwani pia wananchi watanufaika na huduma
za ugani.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.