ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, September 25, 2017

PANGA WAGOMBEA CCM LAWADIA.

MWENYEKITI WA CCM, JOHN MAGUFULI.

KAMATI Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinakutana wiki hii katika vikao vya kuchuja majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ngazi za Wilaya.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, ilieleza kuwa Kamati Kuu itakutana keshokutwa na Alhamisi, na Halmashauri Kuu ya Taifa itakaa Jumamosi na Jumapili.

‘Panga’ hilo litawagusa zaidi wagombea ambao wameanza kampeni mapema kabla ya muda uliopangwa, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona, na wagombea wanaodaiwa kutoa rushwa, ili kupigiwa kura.

Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM, alieleza kukerwa na baadhi ya mambo yanayofanywa na baadhi ya viongozi ndani ya chama hicho na kuapa kukisafisha wakati akikabidhiwa nafasi hiyo na mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete Julai 23, mwaka jana.

Aidha, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo alisema Jumanne iliyopita kuwa kanuni za chama hicho zinawataka wagombea kuchukua fomu kimya kimya, ili wananchi wachague wagombea wanaoona wanafaa kuwaongoza badala ya kuwahadaa kwa mbwembwe na rushwa.

“Taarifa zote tunazo, kama kuna mgombea anadhani anaweza kuanza kampeni mapema na asijulikane tumpe pole maana yanayofanyika huko kote mikoani tunayapata na nawahakikishia watakatwa,” alisema Bulembo kuashiria baadhi ya wanaCCM 'watalia' wiki hii.

Dalili kuwa uchujaji wa wagombea katika chaguzi za CCM mwaka huu utakuwa si wa kiwango cha kilichozoeleka ziliongezwa pia na salamu za Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana wakati wa maandhisho ya miaka 40 ya chama hicho mjini Dodoma.

Kinana alisema wakati wa uchaguzi viongozi wamegeuza kuwa mradi wa kujipatia fedha hivyo kuongeza rushwa kuwa kigezo kingine kitakachoondoa wanachama kwenye orodha ya wagombea.

Taarifa iliyotolewa jana na Polepole ilieleza kuwa vikao hivyo vitakaa kwa mujibu wa ratiba yake ya kawaida, pamoja na mambo mengine vitakuwa na kazi ya kujadili, kupitisha na kufanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea wa CCM walioomba dhamana ya uongozi katika ngazi ya Wilaya.

"Chama Cha Mapinduzi kinapenda kuujulisha umma wa wanachama wa CCM na Watanzania kwa ujumla kwamba vikao vya uongozi vya taifa, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, na Halmashauri Kuu ya Taifa vitakaa hivi karibuni," ilisema taarifa ya Polepole.

Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa vikao hivyo vitafanyika katika Jiji la Dar es Salaam.

CCM ndiyo chama tawala ambapo katika Uchaguzi Mkuu uliopita, mbali na kushinda nafasi ya urais, katika majimbo 264 yaliyopo nchi nzima kilipata majimbo 195 sawa na asilimia 73.86 na kati ya kata 3,946 CCM ilishinda kata 2,875 sawa na asilimia 72.68.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.