HOSPITALI ya Rufaa ya Bugando (BMC) imesema inategemea kumaliza malalamiko ya muda mrefu ya wagonjwa wanaotibiwa kupitia mfumo wa bima ya afya waliyokuwa wakifika hospitalini hapo kupata huduma na kulalamikia utoaji wa huduma wa bima, sio rafiki.
BMC inatarajiwa kuzindua jengo litakalokuwa linawahudumia wagonjwa wa bima ya afya wanaokadiliwa kufikia 800 kwa siku ili kuondoa malalamiko yaliyokuwepo awali kwa wagonjwa wanaotumia bima ya afya.
Kauli hiyo imetolewa leo na Dk. Abel Makubi, Mkurugenzi Mkuu wa BMC, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa jengo hilo linalotarajiwa kuzinduliwa Agousti 25 mwaka huu na Waziri wa afya, Jinsia, Wazee na watoto, Ummy Mwalimu.
Dk. Makubi amesema kuwa, pamoja na kuzinduliwa kwa jengo hilo leo litakakuwa linahudumia wagonjwa wenye kadi kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) huku akidai Wananchi watakaofika hospitalini hapo watapimwa baadhi ya magonjwa bure.
Magonjwa yatakayopimwa bure ni pamoja na shinikizo la damu, magonjwa ya sukari, ukimwi, figo na saratani ya kizazi na matiti ili kutoa fursa kwa wakazi wa mikoa hiyo kufahamu afya zao.
"Lengo ni kuboresha huduma katika hospitali yetu, pia kuhakikisha wagonjwa wanaopata huduma kupitia mfuko wa bima ya afya wanapata huduma kwa wakati mwafaka na watu wengi hawana bima," amesema Dk. Makubi.
Kelebe Luteli, Mkuu wa Kitengo cha Bima, amesema katika jengo hilo litakuwa na sehemu maalumu kwa viongozi wa kitaifa na kimkoa na kwamba madaktari bingwa wa watoto na wakina mama na wa upasuaji watapatikana muda wowote.
"Hapa huduma zote zitapatikana, hii itasaidia ule usumbufu uliyokuwepo kwa wagonjwa wa bima watu walikuwa wanapata huduma kwa usumbufu mkubwa na sasa watafika na kupata huduma kwa wakati mwafaka na kuondoa malalamiko yaliyokuwepo," amesema Luteli.
Hospitali ya Rufaa Bugando yenye vitanda zaidi ya 900 vya kulaza wagonjwa na inayohudumia watu Milioni 14 wa mikoa nane ya kanda ya ziwa na magharibi ilianzishwa mwaka 1971 na kuzinduliwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere (Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.