Muungano mkuu wa upinzani nchini NASA,
hatimaye leo umemtangaza mgombea wake wa urais aliyekuwa akisubiriwa kwa
muda mrefu. Muungano huo umemtangaza kiongozi wa chama cha ODM Raila
Odinga kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika
Agosti 8 mwaka huu.
Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Odinga, mwenye umri wa miaka 72 kuwania urais wa Kenya.
Katika
hafla iliyofanyika kwenye uwanja wa kihistoria wa Uhuru Park jijini
Nairobi na kuhudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa muungano huo, Raila
alitajwa kuwa mgombea urais wa NASA na Kalonzo Musyoka mgombea wake
mwenza ili kuchuana na Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa
Agosti 8.
Katika
hotuba aliyotoa baada ya kuteuliwa, Raila Odinga ameahidi kushusha bei
za vyakula na kupambana na ufisadi. Aidha ameahidi kuifanyia mabadiliko
sekta ya umma na kuwepo serikali za mitaa zenye nguvu zaidi.
Hata hivyo
kutokana na muundo wa mgao wa madaraka uliopangwa na muungano wa NASA,
Raila hatokuwa na madaraka mutlaki endapo atachaguliwa kuwa rais mpya wa
Kenya katika uchaguzi mkuu wa tarehe 8 Agosti.
Vinara wa NASA. Kutoka kushoto: Moses Wetangula, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi. |
Katika muundo huo, kiongozi wa chama cha Amani Musalia Mudavadi atakuwa Waziri Kiongozi anayehusika na Uratibu wa Serikali.
Naye kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula atakuwa Naibu Waziri Kiongozi anayehusika na uratibu wa sekta ya uchumi. Kiongozi wa Chama cha Mashinani Isaac Ruto, atakuwa Naibu mwengine wa Waziri Kiongozi, atakayehusika na utawala na uratibu wa sekta ya huduma za jamii.
Muundo huo wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya vyama tanzu vinavyounda muungano wa upinzani wa NASA unaonyesha kuwa rais atagawana madaraka na washirika wake wakuu ikiwemo katika suala la uteuzi wa baraza la mawaziri kupitia mashauriano na makubaliano
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.