MWANAFUNZI wa chuo kikuu aliyetekeleza mauaji dhidi ya waumini wa Kiislamu waliokuwa wakisali katika msikiti mmoja mjini Quebec nchini Canada siku chache zilizopita ni mtu mwenye misimamo ya mrengo wa kulia na mfuasi sugu wa Donald Trump, Rais wa Marekani.
Kwa mujibu wa machapisho kadhaa katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Alexandre Bissonnette mwenye umri wa miaka 27 amekuwa akitangaza wazi wazi kuwa anaunga mkono misimamo ya chuki dhidi ya Waislamu ya Trump, na pia vuguvugu linalotaka eneo la Quebec lijitenge na Canada la Parti Quebecois.
Mwanachuo huyo amekuwa akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa, anafurahishwa sana na misimamo ya Marine Le Pen, mwanasiasa wa mrengo wa kulia wa Ufaransa ambaye amekuwa akipigia debe sera za chuki dhidi ya Waislamu na wahamiaji nchini humo.
Aidha kijana huyo aliyetekeleza mauaji hayo ya kutisha anadaiwa kusema kuwa analipenda jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel ambalo kila uchao linaua shahidi wananchi madhulumu wa Palestina.
Alexandre Bissonnette ambaye anakabiliwa na mashtaka sita ya mauaji, alipandishwa kizimbani jana Jumatatu katika mji wa Quebec nchini Canada, ambapo mahakama imeagiza awekwe rumande hadi kesi dhidi yake itakaposikizwa tena Februari 21.
Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu mjini Quebec kilisema waumini sita wa Kiislamu waliuawa walipokuwa wakisali Sala ya Ishaa Jumapili usiku, baada ya mwanachuo huyo na mwenzake aliyetoweka kuvamia msikiti huo na kuwamiminia risasi.Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.