Katika msako huo majambazi wanne wamenaswa huku wengine wawili wakiuawa.
Jeshi la Polisi, Kanda ya Ziwa linawashikilia watoto 11 wenye umri wa kuanzia miaka sita hadi 14 waliokutwa kwenye nyumba moja wilayani Nyamagana ambako askari waliivamia kwa lengo la kukamata watu waliowahisi kuwa ni majambazi.
Mmoja wa watu watatu waliokutwa kwenye nyumba hiyo, alitoroka baada ya kurusha bomu la mkono, kabla ya polisi kudhibiti waliosalia kwa kushirikiana na wanakijiji.
Tukio hilo ni mwendelezo wa matukio ya watoto kukutwa kwenye mazingira tata yanayodhaniwa kuwa na uhusiano na mafunzo ya ugaidi au uhalifu. Pia limetokea wakati idadi ya watoto wanaotangazwa kupotea ikizidi kukua.
Mwaka jana watoto 18 kutoka mikoa tofauti walikutwa kwenye nyumba moja mkoani Kilimanjaro ambako walikuwa wanafundishwa dini na ushonaji, na wiki moja baadaye watoto kumi na moja walikutwa kwenye nyumba moja, tukio ambalo liliumiza vichwa polisi.
Mwezi uliopita, polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam waliwakamata wanawake wanne na watoto wanne waliokuwa wamefichwa kwenye kambi iliyopo Kilongoni, Vikindu mkoani Pwani wakidaiwa kufundishwa jinsi ya kutumia mambo ya dini na harakati za ugaidi.
Katika matukio mawili ya Mwanza na jingine la mkoani Shinyanga yaliyotokea usiku wa kuamkia jana, polisi wameua watu watatu na kukamata wengine kumi na moja.
Pia jeshi hilo limekamata bunduki mbili aina ya SMG na AK 47zikiwa na magazine saba na bastola moja zote zikiwa na risasi 183 katika matukio hayo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.