Mbegu bora za pamba. |
NA ANNASTAZIA MAGINGA, Mwanza
WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, ameziagiza taasisi za utafiti za Ukiriguru na Ilonga, Bodi ya pamba na sekta binafsi kumaliza tatizo la ubovu wa mbegu za pamba na kuhakikisha ifikapo mwaka 2019 zinatumika zilizo bora.
Waziri Tizeba ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa zao la pamba jijini Mwanza juzi kwenye mkutano wa 12 baada ya kuwepo kwa idadi ndogo ya mbegu kiasi cha tani 800 huku mahitaji ya wakulima yakiwa tani 23,000 kwa msimu unaotarajia kuanza hivi karibuni mkoani Geita.
Amesema ifikapo mwaka 2019 mbegu bora zianze kutumika nchi nzima ili kuongeza tija kwenye zao hilo na kwamba baada ya kufanyika mabadiliko katika mfumo wa soko na muundo wa Bodi ya Pamba ulisababisha uzalishaji wa mbegu bora kupungua, hivyo wakulima kutonufaika.
“Mbegu zinazotolewa na watafiti haziwafikii wakulima kwa muda muafaka, kwa mfano, mbegu ya UK91 ilitolewa mwaka 1991, leo ni miaka 25 bado mbegu hiyo inapandwa, sote tunafahamu kwamba kwa kuzungusha mbegu kwa miaka mingi hupoteza sifa zake zikiwemo za ubora, uzaaji na ukizani wa wadudu na magonjwa,” amesema Dk. Tizeba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Marko Mtunga, amethibitisha kuwa kwa msimu huu hawana mbegu za kutosha, hivyo wanapambana kuhakikisha mbegu zinapatikana kwa ajili ya wakulima na kwamba bodi imetenga wilaya ya Igunga mkoani Tabora kuzalisha mbegu bora ili miaka ijayo kusiwe na tatizo hilo.
Aidha Waziri huyo amezitaka kampuni za pamba kujiandaa kuwekeza katika kuongeza thamani ya zao hilo kwa kuhamia kwenye biashara ya kutengeneza nyuzi na nguo badala ya kuendelea kuuza pamba ghafi za nje ya nchi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.