Je, Simu za Mkononi Zina Faida au Hasara?
MIAKA kadhaa iliyopita, ungeweza kutumia simu ya mkononi ikiwa ulikuwa na nguvu za kuibeba au ikiwa ilikuwa imeunganishwa na mfumo wa gari lako, kwani betri zake zilikuwa nzito sana. Simu hizo zilikuwa kubwa kuliko boksi za viatu, nazo ziligharimu maelfu ya dola.
Leo kuna simu za mkononi bilioni 1.35 hivi. Katika nchi fulani, zaidi ya nusu ya wakaaji wana simu hizo. Simu nyingi za mkononi zinaweza kutoshea kwenye kiganja cha mkono wako, na nyakati nyingine unaweza kupewa simu ya mkononi bila malipo.* Jarida The Bulletin la Australia linaripoti hivi: “Idadi ya simu za mkononi zinazotumiwa inakaribia jumla ya idadi ya televisheni na kompyuta.” Katika nchi zaidi ya 20, idadi ya simu za mkononi inapita idadi ya simu za waya. Mtaalamu mmoja alisema kwamba zaidi ya kuwa hatua kubwa ya kiteknolojia, simu za mkononi “zimebadili jamii.”
Simu za mkononi zimeleta mabadiliko gani katika jamii? Je, zimeleta faida au hasara?
Zinafaidi Biashara
Biashara nyingi zinafaidika kwa kuwa simu nyingi za mkononi zinauzwa. Shirika moja kubwa lilisema hivi: “Simu ya mkononi ndicho kifaa cha elektroni kinachouzwa kwa wingi zaidi.” Basi, leo watu wanatumia pesa nyingi zaidi kununua simu za mkononi ikilinganishwa na pesa walizotumia zamani kununua kifaa chochote kile cha elektroni.
Kwa mfano, zaidi ya watu milioni 15 kati ya wakaaji milioni 20 wa nchi ya Australia wana simu za mkononi. Katika kipindi cha mwaka mmoja hivi majuzi, wateja wa kampuni moja ya simu za mkononi kati ya kampuni nyingi za simu zilizo nchini humo walipiga simu bilioni 7.5. Kampuni za simu ulimwenguni hupata mabilioni ya dola kwa mwaka kutokana na simu za mkononi. Basi si ajabu kwamba makampuni makubwa huona simu za mkononi kuwa zenye faida.
Kubuni Lugha Mpya
Mara nyingi watu wanapowasiliana kwa simu za mkononi hawazungumzi bali wao huandika ujumbe. Badala ya kuzungumza kwa simu, watu wengi wanaotumia simu za mkononi, hasa vijana, hutuma ujumbe mfupi. Kwa njia hiyo, wao huandika na kutumiana ujumbe mfupi kwa bei nafuu.
Kwa kuwa mawasiliano hayo huhusisha kuandika ujumbe kwa kutumia vibonyezo vidogo vya simu, wale wanaofanya hivyo hufupisha maneno kwa kuchanganya herufi na nambari ili kutokeza ujumbe unaoweza kutamkwa. Ijapokuwa njia hiyo ya kuwasiliana si rahisi ikilinganishwa na kuzungumza kwa simu, kila mwezi ujumbe bilioni 30 hutumwa ulimwenguni pote.
Ni habari gani zinazotumwa kupitia simu hizo? Uchunguzi mmoja uliofanywa nchini Uingereza ulionyesha kwamba asilimia 42 ya vijana kati ya umri wa miaka 18 na 24 hutuma ujumbe mfupi kwa simu ili kuchezeana kimapenzi, asilimia 20 hutuma ujumbe ili kupanga kukutana na watu wa jinsia tofauti, na asilimia 13 wametuma ujumbe ili kuvunja uhusiano.
Baadhi ya watu wanaochunguza hali za kijamii wanahofu kwamba njia ya kuandika maneno na lugha inayotumiwa katika ujumbe mfupi inaathiri uwezo wa lugha wa vijana.
Wengine hawakubaliani na maoni hayo kwani wanasema kwamba njia hiyo ya kuwasiliana “imechochea tena upendezi wa kuandika katika kizazi kipya.” Msemaji wa shirika ambalo hutayarisha kamusi moja ya Kiaustralia aliliambia gazeti Sun-Herald hivi: “Si kawaida kupata nafasi ya kubuni [lugha] mpya . . . ujumbe wa simu na intaneti huwafanya vijana waandike sana. Inawabidi wawe wenye ufasaha ili watambue na kujifunza maneno . . . yanayotumiwa sana.”
Mambo Fulani Yasiyopendeza
Ingawa simu ya mkononi ni kifaa chenye faida katika mawasiliano ya kirafiki na ya kibiashara, kifaa hicho huwafanya wafanyakazi wengi wahisi kwamba wamefungiwa ofisini.
Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba asilimia 80 ya watu wanaofanya matangazo ya biashara na asilimia 60 ya wajenzi huona ni lazima wawe na simu za mkononi kila wakati ili wapokee simu kutoka kwa waajiri au wateja wao.
Watu huona ni lazima wapokee simu haidhuru wako wapi au wanafanya nini, na mtafiti mmoja alifafanua tabia hiyo kuwa “tabia ya mvurugo.” Ili kukabiliana na tatizo hilo, wataalamu wa mambo ya ujenzi wamebuni kifaa cha ujenzi kinachoweza kuzuia mawimbi ya redio ya simu za mkononi kitakachotumiwa katika kujenga mikahawa na majumba ya sinema.—Ona sanduku “Madokezo ya Kutumia Simu ya Mkononi.”
Zaidi ya kuwavuruga watu, simu za mkononi zinaweza kuhatarisha umma. Uchunguzi uliofanywa huko Kanada ulionyesha kwamba kutumia simu ya mkononi unapoendesha gari ni hatari sana kama vile kuendesha gari ukiwa umekunywa kileo.
Profesa Mark Stevenson, wa Kituo cha Utafiti wa Majeraha katika Chuo Kikuu cha Western Australia, anasema kwamba ni vigumu kuzungumza na mtu kwa simu unapoendesha gari kuliko kuzungumza na mtu aliye ndani ya gari hilo.
Licha ya hatari hizo na uwezekano wa kutozwa faini na polisi, uchunguzi uliofanya hivi karibuni ulionyesha kwamba dereva 1 kati ya madereva 5 huko Australia alituma ujumbe mfupi wa simu na thuluthi moja walipiga au kupokea simu walipokuwa wakiendesha gari.
Usafiri wa ndege pia unaathiriwa na matumizi mabaya ya simu za mkononi. Ijapokuwa nyaya za ndege za kisasa zimekingwa zisiathiriwe na mawimbi ya redio ya simu za mkononi, ndege za zamani zinaweza kuathiriwa.
Gazeti New Scientist linaripoti: “Majaribio yaliyofanywa katika ndege mbili na Shirika la Usafiri wa Ndege la Uingereza yamethibitisha kwamba mawimbi ya simu za mkononi huathiri mitambo muhimu ya ndege.” Msemaji mmoja wa shirika hilo alionyesha hatari moja kubwa inayosababishwa na simu za mkononi aliposema hivi: “Simu ya mkononi hutoa nguvu nyingi zaidi kadiri inavyokuwa mbali na kituo cha kurusha na kupokea mawimbi.
Hivyo, kadiri ndege inavyozidi kupaa ndivyo mawimbi ya simu yanavyozidi kuwa na nguvu na hilo huathiri zaidi mitambo ya ndege wakati muhimu sana.” Uchunguzi mmoja uliofanywa huko Australia ulionyesha kwamba katika visa kadhaa vifaa vya elektroni vinavyotumiwa na watu binafsi, kutia ndani simu za mkononi, viliathiri mitambo ya ndege zilipokuwa hewani kwa sababu abiria walipuuza maonyo ya kuzima vifaa hivyo walipokuwa ndani ya ndege.
Simu za Mkononi na Kansa
Bado kuna maoni tofauti-tofauti kuhusu ikiwa mawimbi ya redio yanayotoka katika simu za mkononi na vituo vya kupokea na kurushia mawimbi hayo yanaweza kuwafanya watu wapate kansa. Kwa kuwa watu wengi sana hutumia simu hizo, hata asilimia ndogo kati yao wakiathiriwa, hilo linaweza kuwa tatizo kubwa la afya. Hivyo, utafiti mwingi wa kisayansi umefanywa ili kuchunguza ikiwa mawimbi ya simu za mkononi huathiri chembe za mwili. Utafiti huo umeonyesha nini?
Kikundi fulani cha wataalamu wanaochunguza simu za mkononi kilitoa ripoti iliyosema: “Kikundi hiki kinaamini kwamba kwa msingi wa uthibitisho uliopo, watu hawapaswi kuhangaika kuhusu matumizi ya simu za mkononi.” Pia gazeti New Scientist liliripoti hivi: “Licha ya habari zenye kuogopesha katika miaka ya karibuni, uthibitisho mwingi uliopo unaonyesha kwamba mawimbi ya redio ya simu za mkononi hayaathiri afya ya mtu. Uchunguzi ambao umeonyesha athari fulani haukuweza kuthibitishwa uliporudiwa.”
Kwa kuwa kuna mashaka kuhusu athari za afya zinazosababishwa na simu za mkononi, mamilioni ya dola zinaendelea kutumiwa kufanya uchunguzi. Kabla ya habari kamili kupatikana, kikundi hicho cha wataalamu kinapendekeza hivi: “Tumia simu [za mkononi] kwa muda mfupi iwezekanavyo.
Tumia simu zinazotoa kiwango kidogo cha mawimbi ya redio. Tumia vifaa vinavyokuwezesha kutumia simu bila kuishika maadamu imethibitishwa kwamba vinapunguza kiwango cha mawimbi.” Pia kikundi hicho cha wataalamu kinapendekeza kwamba “watoto walio na umri wa chini ya miaka kumi na sita wasiruhusiwe kutumia simu za mkononi,” kwani “ni rahisi kwao kuathiriwa kiafya na matatizo yasiyojulikana” kwa kuwa mfumo wao wa neva unaendelea kukua.
Licha ya maoni tofauti-tofauti, simu za mkononi zinabadili sana uchumi na hali ya jamii. Sawa na vifaa vingine vya elektroni kama vile televisheni na kompyuta, tunaweza kutumia simu za mkononi vizuri au tunaweza kuziruhusu zitutawale. Uwezo wa kutumia simu za mkononi kwa faida au kwa hasara umo mikononi mwetu.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.