Mama Maria Tereza akisisitiza jambo wakati akitoa shukrani zake kwa wanawake wa Tanzania wanaofanya miradi mbalimbali ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
MAKAMU wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandes de la Vega Sanz (67), amesema kwamba amefurahishwa mno na mafanikio ya wanawake 15 wa Tanzania katika kipindi kifupi baada ya mafunzo waliyoyapata jijini Madrid mapema mwaka huu.
Akizungumza wakati wa chakula cha usiku alichowaandalia akinamama hao wanaotekeleza mradi wa Green Voices katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam usiku huu mara baada ya kutua kutoka Hispania, Mhe. Maria Tereza amesema amefarijika kuona wazo lake lililoibuka mwishoni mwa mwaka 2015 la kuwawezesha wanawake kupambana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi limeweza kuzaa matunda.
Mama Maria Tereza ndiye anayefadhili miradi hiyo kupitia taasisi yake ya Women for Africa Foundation.
“Ni mwaka jana tu mwishoni nilipowaza namna ya kuwawezesha wanawake, hasa wa Tanzania, katika vita ya dunia ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, lakini nafarijika kusikia kwamba wanawake wachache ambao tuliwapatia mafunzo nchini Hispania leo hii wameweza kufanikiwa kuliko hata tulivyotarajia, ni muda mfupi na mafanikio ni makubwa,” alisema.
Mama Maria Tereza alikuwa makamu wa rais wa Hispania kati ya Aprili 18, 2004 hadi Oktoba 20, 2010, na ndiye alikuwa msemaji wa serikali ya Waziri Mkuu Jose Luis Rodriguez Zapatero. Yeye ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya Hispania.
Katika hafla hiyo, Mratibu wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, amesema kwamba ukiacha wanawake watano wanahabari, wanawake 10 wanaotekeleza miradi mbalimbali wameweza kuwaelimisha wanawake wengine 250 mpaka sasa ambao wako kwenye vikundi mbalimbali katika mikoa sita ya Tanzania Bara.
Bi. Secelela amesema kwamba, mafanikio hayo yanatia moyo hasa kutokana na serikali nayo kuunga mkono jitihada hizo za wanawake nchini.
“Kila mradi unaonekana kuigusa jamii moja kwa moja na tunashukuru kuona kwamba viongozi mbalimbali wa serikali wanaitikia na kuwaunga mkono akinamama hawa,” alisema.
Kwa upande mwingine, Dk. Sophia Mlote, ambaye anatekeleza mradi wa kilimo endelevu cha nyanya (Green House) Kinyerezi jijini Dar es Salaam, amesema changamoto pekee ni gharama za kuendesha miradi hiyo hasa mtaji anzilishi, kwani ingawa akinamama wengi wanajifunza, lakini wanashindwa kuanzisha kutokana na uwezo mdogo.
Ameiomba serikali na wahisani kuangalia namna ya kuwawezesha akinamama hao na jamii nzima kwa ujumla, huku akisisitiza kwamba, lengo siyo tu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, bali ni chanzo kikubwa cha ajira kwa wanawake na taifa kwa ujumla.
Mama Maria Tereza Fernandes de la Vega Sanz (kushoto) akimkabidhi zawadi Balozi Getrude Mongella katika hafla hiyo.
Mama Maria Tereza akimkumbatia Balozi Mongella.
Mratibu wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, akieleza jambo wakati wa hafla hiyo.
Mama Mariam Bigambo (kulia) akimvisha mkufu wa shanga Mama Maria Tereza kama zawadi ya wanawake hao.
Ana Salado (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Regina kwa niaba ya wanawake wa Tanzania.
Balozi Getrude Mongella (kulia) akifafanua jambo kwa Makama wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza.
Baadhi ya washiriki wa mradi huo wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Mama Edda Sanga (wa pili kulia mstari wa mbele).
Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza, akijisevia chakula.
Regina, mmoja wa washiriki wa miradi iliyo chini ya Green Voices, akipakua supu ya uyoga.
Akinamama wakiwa pamoja na wageni kutoka Hispania.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.