ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, May 19, 2016

KIKONGWE ALIA AKIOMBA MSAADA

Gonjwa linalomtesa Bibi Rose Shilinde.

DAR ES SALAAMA: “Naishi kwa kula, kunywa kwa kutumia mrija! Ni matatizo juu ya matatizo kwa kweli. Yaani nateseka sana mimi jamani,” hiyo ni sauti ya unyonge wenye kukata tamaa iliyotoka kinywani mwa bibi Rose Shilinde, 60, (pichani) mkazi wa Nyahanga wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga anayesumbuliwa na kansa ya koo iliyosababisha kuvimba kwa mdomo kama anavyoonekana pichani.

Akizungumza kwa shida na Amani huku akisaidiwa na mjukuu wake, Neema Kelya, bibi huyo mwenye watoto tisa aliozaa na mumewe ambaye kwa sasa ni marehemu alisema kuwa, mwishoni mwa mwaka 2015 alianza kusumbuliwa na jino upande wa kulia na tatizo hilo likamsababishia maumivu sambamba na kuvimba mdomo.


MSIKIE MWENYEWE
“Watoto wangu walinipeleka Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kwa ajili ya matibabu ya jino. Lakini madaktari waliponipima waligundua kuwa nina kansa ya koo iliyofika hadi mdomoni.

“Waliniambia ili kupata tiba kikamilifu niende Hospitali ya Taifa, Muhimbili. Ilikuwa mwaka huu mwezi wa tatu, walinipa rufaa ya Muhimbili,” anazungumza bibi Rose na kupokelewa na mjukuu wake baada ya yeye kushindwa kuendelea kutokana na maumivu.

“Tulimfikisha bibi Muhimbili akiwa bado amevimba mdomo. Walipomchunguza, wakatoa majibu kama tuliyopewa Bugando kuwa anasumbuliwa na maradhi ya kansa ya koo hivyo matibabu yake yataanza baada ya wiki mbili mbele na kuendelea hivyo turudi muda huo.”

WARUDI SHINYANGA KWA KUKOSA NDUGU DAR
“Baada ya kuona matibabu ya yataanza muda huo na hatuna ndugu Dar es Salaam, ilitubidi turudi Kahama ili kusuburi siku kama tulivyopangiwa.”

WASHINDWA KURUDI MUHIMBILI
“Kikubwa ambacho ni tatizo kwetu ni kwamba, tulishindwa kurudi Muhimbili kama walivyotuambia baada ya wiki tatu kwa sababu ya kukosa nauli, hivyo tupo tu huku tumemwachia Mungu,” alisema Neema.

HALI YA BIBI HUYO KWA SASA
Neema anasema kuwa, kwa sasa hali ya bibi yake bado mbaya kwani hawezi kukaa kwa muda mrefu. Upande wa chakula, inabidi ale vile vyenye kimiminika, kama maziwa, uji au ndizi lakini zilizosagwa ili kumwezesha kupita kirahisi kwenye koo kwa vile anatumia mrija.

OMBI KWA JAMII
“Tunaomba msaada kutoka kwa jamii itakayoguswa na habari hii ya bibi. Kuna sindano anazotakiwa kuchomwa kwa ajili ya tiba yake lakini inashindikana kwa sababu hatuna uwezo wa kifedha.
“Siku zinavyozidi kwenda, mdomo wa bibi unazidi kuvimba, maumivu ndiyo usiseme. Mimi mwenyewe huwa nalia ninapomwona anavyolalamika, utasema mtoto mdogo,” alisema Neema.

Kwa yeyote aliyeguswa na tatizo la bibi huyu anaweza kumsaidia kupitia simu 0767 118 559 – Neema. Kutoa ni moyo wa kuguswa na wala siyo utajiri.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.