ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, May 27, 2016

APIGWA JIWE NA KUFA KISA KUMWAGA POMBE BAA.

TARIME.

Mkazi wa Kijiji cha Matongo, Kata ya Matongo-Nyamongo wilayani hapa, Mkoa wa Mara, Samwel Kesocho (35), amefariki dunia baada ya kupigwa jiwe kisogoni kwa madai ya kuanzisha fujo baa.


Kaimu Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Sweetbert Njewike alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 23, saa tano usiku katika baa ya Magaigwa Bukima iliyopo Mtaa wa Makaranga.

Njewike alisema, inadaiwa Kesocho alipigwa na jiwe hilo lililorushwa na mtu mmoja.

Alisema majeruhi huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya KMT Shirati wilayani Rorya.

“Chanzo cha ugomvi huo kilisababishwa na Kesocho kuanzisha fujo na kumwaga vinywaji vya wateja,” alisema Njewike.

Kamanda alisema muuaji alikimbia baada ya tukio hilo na kwamba hadi sasa hajapatikana.

Kilo 200 za bangi zakamatwa

Wakati huohuo; Mkazi wa Kijiji cha Sirari wilayani Tarime, Clement Marwa (42) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa akisafirisha kilo 200 za bangi na 20 za mbegu za dawa hizo za kulevya kwenye gari aina ya Toyota Probox alilokuwa akiendesha.

Njewike alisema polisi pia walimkamata raia wa Kenya, Janeth Nyamhanga (49) baada ya kumkuta akisafiri katika gari hilo.

Njewike alisema tukio hilo lilitokea Mei 25, saa tisa mchana katika Mtaa wa Kemange, Kata ya Nyandoto wakati mtuhumiwa akiendesha gari.

Kamanda huyo alisema bangi hiyo na mbegu hizo zilikutwa kwenye vifurushi vilivyofungwa kwa gundi nyeusi. “Watuhumiwa wote wamekamatwa na watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili,” alisema kamanda huyo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.