Na
Emmanuel J. Shilatu
Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Rais Magufuli ni mkwapuaji wa
sera za Chadema lakini hana uwezo wa kuzitekeleza kwa vitendo kwani anatokana
na chama chenye misingi ya wizi na Serikali yake haiwezi kuwa safi na ataishia
kufanya maigizo ya utumbuaji majipu!!
Kauli
hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Chadema Visenti Mashinji wakati akifungua
kongamano la Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) na Umoja wa Wana Chadema Vyuo
Vikuu (CHASO) mjini Dodoma.
Maana
nyepesi ya neno “Mkwapuaji” ni mporaji ambapo Chadema wanataka kuuaminisha umma
kuwa anachokifanya Rais John Pombe Magufuli kimetoka hewani ama ni sera zao
lakini wanasahau Magufuli ameingia Ikulu kutokana na kufaulu kunadi vyema
mkataba na Wananchi ujulikanao kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambazo ndizo sera
zenyewe anazozitekeleza leo hii. Hapo utasemaje Magufuli ni mkwapuaji wa sera
za Chadema zilizokataliwa na Wananchi kupitia sanduku la kura na kuacha
kutekeleza sera za chama chake (CCM) zilizokubaliwa na kumpeleka Ikulu?
Chadema
wanajivika joho la wapambanaji wa ufisadi nchini angali midomo yao imejaa punje
za ufisadi. Tuweke kumbukumbu sawa katika kulithibitisha hili; Chadema
wanapokea ruzuku ya takribani Tsh. Milioni 500 kwa kila mwezi toka kwa ofisi ya
msajili wa vyama vya kisiasa nchini! Lakini leo hii wanashindwa hata kuwa na
ofisi za vyama vyao iwe ni mikoani, wilayani au hata kwenye kata na hao hao
ndio watu wanaopokea mamilioni ya pesa kila mwezi na hao hao hawaonyeshi kwa
jamii matumizi ya pesa hizo. Pesa hizo zinapokwenda hazijulikani, hapo
watajiitaje wapambanaji wa ufisadi nchini wakati wao wenyewe ni lebo ya
ufisadi?
Weka
pembeni hilo la ruzuku, tumulike zile pesa za msaada wanazopewa na mfadhili wao
ambaye ni mfanyabiashara mkubwa Mustapha Sabodo ambapo aliwapa pesa za kuchimba
visima kwenye kila jimbo lenye mbunge wa Chadema, akawapa pesa za ujenzi wa ofisi ya makao makuu ya
Chadema lakini mpaka leo hakuna cha ofisi wala kisima kilichochimbwa. Wanapata wapi
ujasiri wa kujiita wapambanaji wa vita ya ufisadi wakati ndani mwao kumejaa “Panya”
wanaotafuna pesa kama mchwa? Hiki kweli utakiita chama kinachopinga vita
ufisadi ama ni Saccoss ya kufa na kuzikana?
Ukweli
unabaki pale pale kwamba CCM ndio waasisi wa vita ya mapambano ya ufisadi
nchini na anayoyafanya Rais Magufuli kwa sasa ya kupambana na ufisadi nchini
kwa kuyatumbua majipu mafisadi yote ni mwendelezo wa urithi toka kwa Marais ama
toka kwa Serikali zilizopita.
Kwa wale wasioelewa Kwenye
katiba ya CCM kifungu cha 1 ibara ya 8(2) inatoa masharti kwa kila mwanachama
kuwa mtu anayefanya juhudi za kuielewa kuieleza na kuitekeleza itikadi na siasa
ya CCM. Hivyo mojawapo ya kazi ya mwana CCM ama kada wa CCM ni lazima awe
mstari wa mbele katika mapigano dhidi ya ufisadi na mafisadi nchini. Hii
haijalishi awe anatoka katika kamati kuu (C.C) ama katika tawi.
Serikali imekuwa ikisikiliza
kupokea na kutimiza wajibu wa utekelezaji wa mambo yote yahusuyo rushwa na
ufisadi nchini kupitia kwa “makomandoo” mbalimbali wa upiganaji wa maovu
nchini.
Tusisahau jinsi gani Chifu
Abdallah Fundi Kira alivyochapwa voboko kutokana na kupokea rushwa ya sh. 25/-.
Pia wahujumu uchumi hawatakaa wamsahau Edward Sokoine kwa jinsi alivyopambana
nao. Haya ndio mapambano ya dhahiri nay a ushahidi wa Serikali za CCM.
Tusimsahau Mzindakaya ‘Mzee wa
Mabomu’ alivyomlipua Idd Simba kwenye sakata la sukari. Pia tumkumbuke
Sokoine na machukizo dhidi ya wahujumu uchumi. Pia tusimsahau Dr. slaa
alipojitoa muhanga kuwataja mafisadi (10 list of shames) wa EPA pale Mwembe Yanga. Tuendelee
kukumbuka harakati za mapigano ya Dialo dhidi ya uwekezaji ndani ya
maliasili.
Yapo mambo mengi mno
yaliyoibuliwa na baadhi ya wanaharakati lakini nayo Serikali haipo nyuma kwenye
uchukuaji wa utekelezaji wa dhahiri wa mapigano dhidi ya ufisadi bila ya
kuangalia hadhi, umaarufu wala wadhifa wake. Pia tumeshuhudia viongozi
waandamizi na makada wakubwa wa chama wakijiuzulu na wengine kulala rumande na
hata kupelekwa mahakamani.
Ila sisi wananchi tu wepesi sana
wa kusahau. Tusisahau kukumbuka jinsi gani watuhumiwa wa EPA wanavyopandishwa
mahakamani pia tu mashuhuda wa jinsi gani vigogo wa BOT walivyosota jela kwa
ajili ya kashfa za magendo pacha, uzidishaji wa utengenezaji wa noti EPA. Jamii pia imeshuhudia watuhumiwa
wa nyara za Serikali za kontena lililokuwa na meno ya tembo waliburuzwa
mahakamani
Tusisahau sakata la minofu ya
samaki na kitita cha sh. Million 900 kule Mwanza akina Mzindakaya na Lamwai
walimpelekea kilio Profesa Mbilinyi hatakaa alisahau hili. Pia tukumbuke
dhoruba iliyompata Aron Chiduo enzi ya utawala wa Mwinyi.
Kwa haya, napenda kuzipongeza
Serikali zote kwa kuonyesha uhai kwenye mapigano dhidi ya rushwa na ufisadi
nchini.
Naam, mtu akifanya vizuri lazima
apewe haki (pongezi) zake tena kwa roho moja. Wale wanaobeza harakati hizi
sijui tuwaweke kundi gani ambalo jamii itawaelewa.
Ni jambo la kushangaza kuona ni
jinsi gani watu ama kundi la watu linavyojipa sifa ambazo sio zao. Mathalani
vyama vya upinzani wanajitutumua kwa kauli zao kwamba wao ndio waanzilishi wa
mapambano ya rushwa na ufisadi nchini.
Rais Magufuli naye pia
ameendeleza mapambano yale yale ya vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini kwa kuyatumbua
majipu sugu wale wote watafunaji wa rasilimali za Taifa na watumiaji madaraka
vibaya kwa maslahi binafsi. Tumeona vigogo wazito kabisa wakikumbwa na tumbua
majipu ya Rais Magufuli pasipo uonevu wala kumuonea haya mtu kwani haya ndio
matarajio ya Watanzania walio wengi kuona yakitendeka. Kama ni upele umempata
mkunaji, John Pombe Joseph Magufuli.
Tumekuwa Taifa la watu vigeugeu
na wapotoshaji, leo hii waliokuwa wakipiga kelele juu ya mafisadi na watu
wanaotumia madaraka vibaya kuwa hawashikiki ndani ya nchi , leo hii watu wale
wale waliokuwa wakipaza sauti za kuona mapambano ya vita ya ufisadi nchini ndio
wamegeuka watetezi wa mafisadi wenyewe.
Rais Magufuli ameendelea
kujionyesha kwamba yeye ni mtendaji haswaa kwani alihaidi kukusanya kodi na
kuziba mianya yote ya ukwepaji kodi ili tuondokane na tatizo la utegemezi na
kuwa ombamba. Leo hii tunayaona matunda ya utekelezaji wake kwani mapato ya
ndani ya nchi yameongezeka kutoka makusanyo ya Bilioni 800 kwa mwezi na hadi
kufikia makusanyo ya trilioni 1.5 kwa mwezi. Huu ni ushahidi wa utekelezaji na
utendaji aliojaaliwa Rais Magufuli.
Rais Magufuli huyu huyu alihaidi
kubana matumizi ya pesa nchini na amekuja kuyaishi maneno yake kwani leo hii
amefanikiwa kufuta posho za ovyo ovyo walizokuwa wanalipana vikaoni, amefuta
safari za nje za viongozi wote na kusafiri ni mpaka upate kibali rasmi,
amefanikiwa kuwafuta watumishi hewa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara pia
amefuta walsha na semina zisizo na tija na badala yake watu wanatakiwa wafanye
kazi tu kwa vitendo na porojo.
Haya mambo yote yameendelea
kuimarisha mapato ya ndani ya nchi na pesa nyingi zimeendelea kuokolewa. Mathalani
hivi karibuni Bunge walifanikiwa kuokoa bilioni 6 fedha walizozikabidhi kwa
Rais Magufuli na yeye kuzielekeza zikatengeneze madawati na hivyo kutaondoa
tatizo la madawati nchini. Nani kama Magufuli?
Jambo
la kufurahisha Rais Magufuli ameonyesha si mkwapuaji wa Sera za chama chochote
kile bali anasimamia sera za chama chake na kuonyesha kwa matendo utumishi na
uwajibikaji wa dhati; Rais Magufuli huyu huyu ameongeza makusanyo na ameonyesha
uwazi katika kutoa taarifa kila mwezi juu ya mapato na matumizi ya makusanyo ya
pesa yanayofanywa na Serikali. Mpaka sasa Rais Magufuli amejionyesha si
mkwapuaji bali ni mtekelezaji, mtendaji, Mzalendo na mchapa kazi mwenye maono
na malengo ya kutuondoa kwenye umaskini.
0717488622
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.