ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, December 3, 2015

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA WATU WENYE ULEMAVU DUNIANI TAREHE 3 DESEMBA 2015, MKOANI MWANZA.

Picha inamuonesha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo akimkabidhi  Katibu wa SHIVYAWATA Mkoa wa Mwanza Alfredy Kapole Rosheni zinazotumiwa na watu wenye ulemavu wa Ngozi Albino. 
Atley Kuni- Afisa habari Mwanza.

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA WATU WENYE ULEMAVU DUNIANI TAREHE 3 DESEMBA 2015, MKOANI MWANZA. 

Mhemishiwa Amon Anastazi Mpanju, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania, 

Mheshimiwa Rabikira O. Mushi, Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii 

Waheshimiwa Wabunge,  Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi, 

Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa, 

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu , na Mashirika ya Watu Watu Wenye Ulemavu, 

Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa, 

Wanahabari na wasanii, 

Wageni Waalikwa, 

 Mabibi na Mabwana. 

2 1.0 Salaam Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania na kamati ya maandalizi chini ya uratibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kunialika niwe Mgeni Rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya hii ya Kimataifa ya watu wenye Ulemavu duniani, ambayo kitaifa inafanyika hapa katika Jiji la Mwanza. 

Ndugu Wananchi; Aidha napenda kuishukuru kamati ya maandalizi, Uongozi wa mkoa wa Mwanza, Taasisi mbalimbali na wadau wa masuala ya Watu Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa jitihada mlizofanya katika kufanikisha maadhimisho haya. 

Hongereni sana!! Ndugu Wananchi; Nina hakika sote tunajivunia siku hii, ambayo kwa pamoja tutaitumia kutafakari juu ya changamoto mbali mbali zinazowakabili watu wenye aina mbalimbali za ulemavu na kuweka mikakati ya 3 pamoja ya kuweza kujenga jamii ya watu walio sawa na huru, inayopinga vitengo vya ubaguzi na unyanyasaji kwa binadamu. 2.0 

Hali ya Watu Wenye Ulemavu Ndugu Wananchi; Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Afya Ulimwenguni ya mwaka 2011, takribani watu wapatao billion 1 ulimwenguni wana changamoto ya ulemavu wa aina mbalimbali. 

Asilimia 80 miongoni mwao wanaishi katika nchi zinazoendelea na zile za uchumi wa kati. Aidha kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina jumla ya watu wenye Ulemavu 2,641,802 sawa na aslimia 5.8 ya wananchi wote; kati yao watu wenye Ualbino inakadiriwa kuwa ni 16, 477 sawa na asilimia 0.04 ya wananchi wote. 

Wasioona ni 848,530 sawa na aslimia 1.93, kusikia 425,322 sawa na aslimia 0.97, kujongea 525,019 sawa na aslimia 1.19, kukumbuka 401,931 sawa na aslimia 0.91, kujihudumia 324,725 sawa na aslimia 0.74 na ulemavu mwingine 99,798 sawa na aslimia 0.23. 

Sababu zinazochangia ulemavu ni pamoja na Urithi, magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, ajali, athari za dawa na pombe pamoja na changamoto katika upatikanaji wa huduma za afya hasa vijijini. 4 3.0 Kauli Mbiu Ndugu Wananchi; Kauli mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu ni “Incusion matters: access and empowerment for people of all abilities. 

Au kwa Kiswahili; Ujumuishwaji ni muhimu: ufikikaji na uwezeshaji kwa watu wenye ulemavu, wanao uwezo wa kutenda mambo ya aina moja au nyingine wakiwezeshwa na kupewa fursa sawa katika jamii.

Kauli mbiu hiyo inaakisi matwaka ya sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 pamoja na sera, miongozo na mipango mbalimbali ya serikali kuhusu huduma za watu wenye ulemavu hapa nchini. 

Aidha, serikali ya awamu ya tano, itahakikisha kwamba haki, ufikiaji na uwezeshaji kwa watu wenye ulemavu nchini vinatekelezwa kwa vitendo. 5.0 Changamoto za Watu Wenye Ulemavu Ndugu Wananchi; Katika risala yenu mmezungumzia changamoto na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kushughulikia changamoto hizo. 

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na upatikanaji wa taarifa kwa viziwi, ukatili na unyanyasaji kwa watu wenye ualbino, kukosekana kwa uwakilishi wa watu wenye ulemavu katika ngazi 5 mbalimbali za maamuzi, kukosekana kwa ofisi ya kudumu ya shirikisho la watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA), miundo mbinu isiyo rafiki kwa watu wenye ulemavu ya majengo mengi yanayotoa huduma kwa umma, kukosekana kwa alama maalumu za barabarani ambazo zingewezesha watumiaji wa barabara kuziheshimu na hivyo watu wenye ulemavu kumudu utumiaji wa barabara, ruzuku ndogo kwa vyama vya watu wenye ulemavu na uratibu wa masuala ya watu wenye ulemavu.

6.0 Utatuzi wa Changamoto Ndugu Wananchi; Serikali imepokea mapendekezo yaliyotolewa katika risala ya watu wenye ulemavu nchini na inaahidi kuyafanyia kazi kwa kuzingatia sheria na sera zinazosimamia utumishi wa umma na utoaji wa huduma mbalimbali za jamii. 

Hata hivyo sina budi kutoa ufafanuzi wa utekelezaji wa masuala yafuatayo: 6.1 Huduma za afya: Ndugu Wananchi; Serikali ya awamu ya tano imejipanga katika kuhakikisha kwamba wananchi wote kutoka makundi mbalimbali ya jamii yanapata huduma bora za Afya bila ubaguzi wala unyanyapaa wa aina yoyote. 

Hatua mbalimbali zitachukuliwa ili kufikia adhma hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati katika kila kijiji, kituo cha 6 afya kwa kila kata, hospitali kwa kila halmashauri na hospitali ya rufaa kwa ngazi ya mikoa. 

Aidha serikali itahakikisha upatikanaji wa wataalamu wa afya katika ngazi zote pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika taasisi hizo za Afya nchini. Vile vile serikali inakamilisha mwongozo wa uchangiaji wa huduma za afya nchini. 

Mwongozo huo utatoa utaratibu mzuri zaidi wa upatikanaji wa huduma kwa makundi maalumu ikiwemo watu wenye ulemavu. 6.2 Ukatili na unyanyasaji dhidi ya watu wenye Ualbino Ndugu Wananchi; Kuanzia mwaka 2006, nchi yetu imekuwa ikikabiliwa na tatizo la kujirudia rudia kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino. Vitendo hivi vinajumuisha mauaji na ukataji wa viungo kwa ndugu zetu Albino. 

Mauaji hayo yamekuwa yakichochewa na sababu mbalimbali zinazoambatana na imani za kishirikina , ambapo baadhi ya watu wanaamini kwamba kiungo cha mtu mwenye ualbino kinaleta bahati kama vile utajiri wa haraka, vyeo au tiba kwa magonjwa sugu kama vile UKIMWI. 7 Ndugu Wananchi; Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea na juhudi mbalimbali za kupiga vita vitendo hivi. Jitidaha hizo zinajumuisha utoaji wa elimu kupitia vyombo vya habari na kampeni za kitaifa. 

Aidha serikali imeunda kamati ya Kitaifa inayosimamiwa na Wizara ya mambo ya ndani ya nchi. Kamati hiyo inaendelea na kazi ya uratibu na kutoa ushauri kwa serikali katika kukabiliana na vitendo hivi viovu. 

Pia serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watu wote wanaoshiriki kufanya vitendo hivi vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Aidha, juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda, kwa kupungua kwa vitendo hivi viovu dhidi ya ndugu zetu Albino. 

Hata hivyo, tusibweteke na mafanikio haya, badala yake juhudi zinapaswa kuongezwa ili tatizo hili liwe historia katika Taifa letu. 

Inawezekana, Timiza wajibu wako!!! 6.3 Miundo mbinu Rafiki ,Utolewaji wa Ruzuku na upatikanaji wa ofisi ya Shirikisho Ndugu Wananchi; Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya ufunguzi wa bunge ya tarehe 20/11/2015 nilizungumzia kuguswa kwangu na matatizo mbalimbali yanayohusu watu wenye ulemavu hususani 8 upatikanaji wa haki zao za msingi.

Napenda kutumia maadhimisho haya kutoa maelekezo kwa Idara mbalimbali za serikali na Mamlaka za serikali za mitaa kuweka mikakati thabiti ya kuondoa kero kwa watu wenye ulemavu ikiwemo ujenzi wa majengo yanayozingatia miundombinu rafiki na alama za barabarani zinazozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu. 

Pia Ofisi za mikoa na Halmashauri ziangalie uwezekano wa kuvisaidia vyama vya watu wenye ulemavu kwa kuwapatia ofisi ili vyama hivyo ziweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. 

Vilevile, vyombo vya habari havina budi kutekeleza sheria ya watu wenye ulemavu kwa kuwaajiri wataalam wa lugha ya alama ili kuwezesha viziwi kupata haki ya kupata taarifa kama ilivyo kwa wananchi wengine. 

Kuhusu suala la ruzuku, serikali ya awamu ya tano itahakikisha kuwa ruzuku inayotolewa kwa vyama vyama vya watu wenye ulemavu itakuwa inatolewa kwa wakati. Aidha serikali itaangalia namna ya kuboresha ruzuku hiyo kwa kuzingatia hali ya uchumi wa nchi. 

Hata hivyo, napenda kutoa angalizo kuwa fedha hizo kidogo mnazopata zitumike kwa makusudio yenye tija ya kuimarisha vyama vya watu wenye Ulemavu nchini. 

Mkumbuke kuwa mnapaswa kutoa taarifa ya matumizi ya fedha hizo serikalini kama ilivyoainishwa katika sheria ya watu wenye ulemavu. 9 6.4 Uratibu na Usimamizi wa masuala ya watu wenye ulemavu Ndugu Wananchi; Serikali imepokea mapendekezo yenu kuhusu ombi la masuala ya watu wenye ulemavu kuhamia katika ofisi ya Waziri Mkuu au ofisi ya Rais. 

Hata hivyo, napenda kutoa ufafanuzi kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwemo watu wenye ulemavu. Hivyo napenda kuwatoa hofu kuwa, Wizara yoyote itakayopewa dhamana ya kusimamia masuala ya ustawi wa jamii, itatimiza wajibu wake wa kutoa huduma kwa mujibu wa sheria na sio kama fadhila. 

Ndugu Wananchi; 7.0 Mwisho Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sijawashukuru kwa burudani murua na maridhawa ambazo zimetoa hamasa kubwa katika maadhimisho haya. Kwa namna ya pekee nimeburudika sana na burudani zilizotolewa na watu wenye ulemavu. Hongereni sana. 

Pia,niwapongeze tena Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Uongozi 10 wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kufanikisha maadhimisho ya siku hii muhimu kwa mustakabli wa Taifa na maisha ya Watu wenye Ulemavu hapa nchini. 

Hivyo, hatuna budi kuitumia siku hii katika kutafakari kwa kina kuhusu changamoto za watu wenye Ulemavu na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kudumisha ulinzi, usalama na ustawi wa kundi hili hapa nchini; kwa malengo ya kujenga jamii jumuishi inayozingatia upatikanaji wa haki kwa makundi yote ya jamii. “Asanteni kwa Kunisikiliza”

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.