ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, December 23, 2015

ABIRIA ASIMULIA KILICHOTOKEA UTEKWAJI WA GARI LA ABIRIA MISUNGWI.

NA PETER FABIAN, MWANZA.
GARI la abiria la Master City lililokuwa likitokea Jijini Dar es salaam kuelekea jijini Mwanza juzi kuamkia jana majira ya saa 7:00 usiku lilitekwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi katika eneo la mpakani mwa Kata ya Igongwa Wilaya ya Kwimba na Mabuki wilayani Misungwi mkoani Mwanza.

Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la tukio zimeeleza kuwa basi hilo lenye namba za usajili T974CDS aina ya Youtong likiendeshwa na dereva wake Joseph Halu lilitekwa na abiria wake kupewa kichapo kisha kuporwa fedha, simu za mkononi, mabegi mepesi na mali zingine za abiria hao waliokuwa wakitokea jijini Dar  kuelekea jijini Mwanza eneo la mpakani mwa Jimbo la Misungwi anakotoka Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga “Mawe matatu”.

Mmoja wa watu watu walioshuhudia tukio hilo, Ruben Nzungu, mkazi wa Hungumalwa akiwa na gari dogo aina ya Noah akisimulia kwa njia ya simu kupitia JEMBE FM mesema kuwa alipofika eneo la daraja la Kijiji cha Bushini mpakani mwa Wilaya za Kwimba na Misungwi aliona lori la mizigo (Sermi- trailer) na mbele ya gari hilo kulikuwa na Basi la Master City likiwa limesimama huku pembeni ikionekana magogo ya miti na mawe yakiwa yamefunga barabara na watu wakimulika tochi. BOFYA PLAY KUSIKILIZA


Nzungu amesema alianza kupata hofu baada ya kupewa ishara na dereva wa lori kubwa la mizigo lililokuwa mbele yake akawasha taa kali (Full-Light) na kuona watu wakiwa wamechuchuma chini huku baadhi yao wakionekana kushika mapanga na wengine marungu ndipo akagundua kuwepo hatari mbele na kufunga breki ili kugeuza gari alilokuwa akiendesha.

“Baada kama ya dakika 5 hivi tukiwa tunatafakari tukaona gari la Askari Polisi likielekea eneo la tukio lakini pembeni kwa mbali tukawa tunaona watu waliokuwa na tochi wakikimbilia na kuishia vichakani, tuliposogea tukakuta Basi hilo limevunjwa viyoo vya pembeni na upande wa dereva na kondakta kwenye mlango wa abiria huku baadhi wakilia kupigwa na marungu na wengine kukatwa mapanga,”alisema.

Shuhuda huyo alieleza kuwa askari Polisi walipokuwa wakiwahoji abiria kama watu hao ambao inadaiwa walikuwa wamefunika nyuso zao mfano wa Ninja walidai kuwa hawakuona watu hao walioingia ndani kuwa na silaha ya moto zaidi ya rungu na mapanga labda waliokuwa wamebaki chini ya gari wakitoa amuri ya kuwataka wenzao kusanya fedha, simu za mkononi na kuchukua baadhi ya mabegi madogo ndani ya gari na kwenye buti.

Mmoja wa abiria ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake alisema kuwa alikuwa kiti cha mbele jirani na dereva, wakiwa wametoka eneo la Hungumalwa (Kwimba) kuelekea Misungwi ghafla njiani majira ya saa 6:50 usiku tulipofika eneo la daraja dereva akapunguza mwendo baada ya kuona magogo ya miti na matawi yakiwa barabarani na aliposimama tu tukasikia mawe yakirushwa madirishani na ghafla kuamuliwa kufungua mlango wa abiria.

“Watu hao walivalia soksi za kuficha nyuso zao na kuanza kutushambulia wakituamuru kutoa fedha, simu za mkononi, wengine wakichukua mabegi na mikoba ya wanawake waliokuwa wakichelewa kuwapa walichodai, pia waliwapiga baadhi ya abiria virungu na baadhi kukatwa na mapanga na wengine kuwaamuru kushuka chini ili kuwanyang’anya vitu ikiwemo saa za mkononi,”alisimulia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Yustus Kamugisha, alipotafutwa kuhusu kuthibitisha tukio hilo kupitia njia simu ya mkononi alituma ujumbe mfupi kuwa yupo kwenye kikao cha makabidhiano kati yake na aliyekuwa RPC Charles Mkumbo ambaye amehamishiwa makao makuu kitengo cha Intelenjensia iliyokuwa chini Valentino Mlowola aliyeteuliwa na Rais Dk John Magufuli hivi karibuni kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.