TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo amekabidhiwa rasmi ofisi na Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohammed Gharib Bilal Ikulu, Jijini Dar es salaam.
Baada ya makabidhiano hayo Mhe. Samia, alikaribishwa na watumishi wa ofisi yake ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii kulingana na kauli mbiu ya 'Hapa ni Kazi tu'.
"Kila mmoja afanye kazi kwa bidii mahala pake pa kazi. Wale ambao kauli mbiu ya Hapa ni Kazi tu, itawapita wakae pembeni... watatusamehe", alisema Makamu wa Rais
Aidha Mhe. Samia alisisitiza suala la kuendelea kupendana na kushirikiana miongoni mwa watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais ili kufanikisha azma ya kuleta matarajio ya maendeleo ya Watanzania wanayotaka kuyaona katika uongozi wa awamu ya tano.
Baada ya kutoa nasaha hizo alifanya kikao na Menenjimenti ya ofisi ambapo alitoa uelekeo wa utendaji kazi katika ofisi hiyo hususan kuzingatia kusimamia masuala ya muungano na mazingira ili kufanikisha malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Aliitaka Menejimenti hiyo kujipanga upya na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa ajili ya kuleta mabadiliko kwa upande wa masuala ya muungano na mazingira.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
9/11/2015
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.