Dar es Salaam. Rais Dk John Magufuli ameingia rasmi Ikulu leo mchana mara baada ya kuapishwa kuanza safari ya uongozi wake kwa miaka mitano.
Rais Magufuli, aliyekuwa ameambata na mkewe Janet, ameingia katika makao yake hayo mapya saa 7:25 mchana akiwa na maofisa wa Ikulu na viongozi wengine wa ulinzi na usalama.
Baada ya kuingia, alipokelewa kwa nyimbo mbalimbali za kumpongeza na kikundi maalumu cha waimbaji waliokuwa wamevalia vyema nguo za rangi ya bluu, njano, nyeusi na kijani zikiwa na picha rais Dk Magufuli.
Hata hivyo, Rais na mkewe walipelekwa moja kwa moja Ikulu na maofisa wa usalama.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema Watanzania wengi wana imani na kiongozi huyo mpya kuwa atawaletea maendeleo, hivyo wajiandae kufanya kazi kwa kuwa kauli mbiu ya kiongozi huyo ni "Hapa Kazi Tu."
"Watanzania wengi walitaka kushuhudia rais anavyoapishwa lakini kutokana na uwanja kuwa mdogo wasingetosha. Tunasikitika hatukuwa na nafasi ya kutosha kwa kila Mtanzania lakini wananchi wengi wana imani Rais Dk Magufuli kuwa atawaletea manufaa makubwa kwa taifa, " amesema Sefue.
Kova anena
Kamishna wa kanda Maalumu ya Kipolisi Dar es Salaam, Suleiman Kova amewataka Watanzania kusahau yaliyopita wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu na kuendelea kulinda amani ya nchi.
Amesema anawashukuru watu wote kwa utulivu wao hadi kipindi ambacho rais ameapishwa na kwamba anamtakia kila la kheri kwenye majukumu yake mapya.
CHANZO: MWANANCHI
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.